1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkosoaji wa rais Museveni aitoroka Uganda

10 Februari 2022

Kutoweka kwa mkosoaji sugu wa utawala wa rais wa Uganda Yoweri Museveni kumepokelewa na umma kwa maoni mseto. Kulingana na wakili wake, Kakwenza Rukirabashaija ametorokea Ulaya katika nchi ambayo bado haijajulikana.

https://p.dw.com/p/46nan
Kakwenza Rukirabashaijav
Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Mkoasoaji huyo ambaye ni mwandishi vitabu wa mtindo wa tashtiti Kakwenza Rukirabashaija alikuwa wa kwanza kusambaza ujumbe kwamba hatimaye aliondoka Uganda bila kibali huku akimkejeli hakimu aliyemnyima kibali chake.

Baadaye mawakili wake wakathibitisha kuwa bwana huyo alikuwa ametorokea Ulaya akipitia Rwanda akielekea nchi moja ya Afrika ambako atakaa siku tatu kabla ya kuelekea Ulaya. Walisisitiza kuwa Kakwenza alilazimika kutoroka ili aende kupata matibabu maalum kufutia majeraha mabaya yaliyotokana na mateso aliyopata akiwa korokoroni.

Kakwenza alikamatwa mwishoni wa mwezi Desemba mwaka uliopita na akazuiliwa bila kuwasiliana na mtu yeyote kwa siku 15. Katika kipindi hicho Kakwenza alisimulia mateso ya kikatili aliyofanyiwa na askari wa vyombo vya usalama.

Baada ya vilio na shtuma kutoka ndani na nje ya nchi, alifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii. Lakini hata baada ya kuachiwa kwa dhamana wiki moja baadaye, mwandishi huyo amekuwa akiwindwa na vyombo vya usalama.

Mateso dhidi ya kakwenza yamefufua mjadala mkali katika bunge la Uganda wiki hii hasa baada ya vyombo vya habari kurusha picha za majeraha na makovu yaliyo kwenye mwili wake. Kwa baadhi ya wanasiasa, vitendo vya kumhujumu mwandishi huyo na wengine wengi ni kielelezo kuwa kuna watu ndani ya utawala wa Museveni ambao wanalenga kumchafulia jina yeye na serikali yake kwa jumla kwamba haiheshimu haki za binadamu.

Kakweza alikuwa ameomba kwenda kutibiwa Ujerumani. Lakini hadi sasa haijathibitishwa kama huko ndiko safari yake bila kibali itamfikisha.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala