Mkuu wa IAEA azuru kinu cha Fukushima nchini Japan
5 Julai 2023Mkuu wa shirika la kudhibiti nishati nyuklia la Umoja wa Mataifa, IAEA, Rafael Grossi amepangiwa kukitembelea kinu cha nyuklia cha Japan kilichoharibiwa na Tsunami leo Jumatano, baada ya shirika analoliongoza kuthibitisha usalama wa mpango tata wa kutiririsha maji yaliochafuliwa na mionzi baharini.
Akiwa njiani kuelekea mtambo wa Fukushima Daiichi, Grossi alihudhuria mkutano wa maafisa wa serikali na kinu hicho, pamoja na mameya na viongozi wa vyama vya wavuvi, na kusisitiza shirika hilo litakuwepo wakati wote wa utiririshaji wa maji hayo ili kuhakikisha usalama na kushughulikia wasiwasi unaoelezwa na wenyeji kilipo kinu cha Fukushima.
Katika ripoti yake ya mwisho iliyotolewa jana Jumanne, IAEA ilihitimisha kuwa mpango wa kutiririsha maji ya kinu cha Fukushima ambayo yamesafishwa kupunguza kiwango cha mionzi hautakuwa na athari kubwa za kimazingira na kiafya.
Lakini mashirika ya ndani ya wavuvi yameukataa mpango huo kwa sababu ya wasiwasi kwamba sifa yao itaathirika hata kama samaki wao hawajachafuliwa. Pia unapingwa na makundi kama Korea Kusini, China na baadhi ya mataifa ya visiwa vya pasifiki kutokana na wasiwasi wa usalama na sababu za kisiasa.