Mkuu wa IMF afikishwa mahakamani kwa tuhuma za uzenbe
12 Desemba 2016Lagarde atafikishwa mbele ya jopo la majaji wanaosikiliza kesi zinazohusiana na makosa ya watendaji wakuu wa serikali kama mawaziri. Jopo hilo hutathmini iwapo mawaziri hao walifanya makosa wakati walipokuwa wanatekeleza majukumu yao. Kwa hali yoyote ile kesi hii itaathiri sana wasifu wake kikazi kwani Lagarde ambaye ni wakili mashuhuri alipanda kupitia ngazi ya wizara ya fedha hadi kufikia kuwa mmoja kati ya wanawake wenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani. Iwapo kweli atapatikana na hatia, basi shirika la fedha duniani IMF litakuwa pia limepata dosari. Lakini mpaka sasa Christine Lagarde amekanusha kufanya makosa yoyote,anadai kuwa yeye alifanya kazi yake kadri ya uwezo wake na kama kwa njia yoyote ile uzembe au ubadhirifu wa fedha umejitokeza basi sio kwa makusudi yake. Wakili wa Lagarde, Patrick Maisonneue amesema hana shaka mteja wake huyo atasimama imara na kujitetea.
Tuhuma zinazomkabili Christine Lagarde zinatokana na madai ya ubadhirifu wa fedha yanayomkabili Bernard Tapie ambaye pia alikuwa waziri. Tapie mwenye umri wa miaka 73 alikuwa anamiliki kampuni ya Adidas kati ya mwaka 1990 na 1993 lakini baadae alilazimika kuiuza kampuni yake hiyo baada ya kufilisika. Benki inayomilikiwa na serikali ya Ufaransa Credit Lyonnais iliinunua kampuni hiyo kwa kiasi cha Euro milioni 315.5 mnamo mwezi Februari mwaka 1993 lakini baada ya mwaka mmoja tu benki hiyo ikaiuza tena kampuni hiyo kwa bei ya Euro milioni 701 hatua ambayo ilimfanya Tapie alalamike na kudai kuwa alidanganywa au alidhulumiwa. Mwaka 2007 Christine Lagarde alipopewa wadhfa wa waziri wa fedha na rais mpya wakati huo Nicolas Sarkozy aliliingilia swala hilo na kulitolea ufumbuzi uliozifanya pande mbili kuafikiana nje ya mahakama, katika makubaliano ambayo yalimfanya Tapie kuwa ni mshindi kwani alilipwa kiasi cha Euro milioni 404 kama fidia. Hata hivyo Tapie alilazimika kuzilipa fedha hizo baada ya kufunguliwa kesi iliyoendelea mahakamani kwa muda mrefu.
Wachunguzi wanashuku kuwa makubaliano hayo yaliyofanyika nje ya mahakama yalimpendelea Tapie kimakusudi kwa sababu alimuunga mkono Nicolas Sarkozy katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2007.
Ijapokuwa Lagarde halaumiwi kwa kufaidika binafsi na fedha hizo lakini analaumiwa kwa kukosa kuzuia malipo hayo.
Mwandishi: Zainab Aziz
Mhariri:Yusuf Saumu