Msaada watiririka India, vifo vya corona vyaongezeka
3 Mei 2021India imeutanua mpango wake wa utoaji chanjo kwa watu wazima, lakini majimbo mengi yanakabiliwa na uhaba wa dozi licha ya zuio la kuuza nje ya nchi chanjo zinazotengenezwa nchini humo. Kuongezeka kwa idadi ya vifo kumetokea wakati vifaa vya matibabu kutoka nchi za kigeni – ikiwemo viwanda vya kuhamishika vya kutengeneza oksijeni – vikisafirishwa katika mji mkuu New Delhi kama sehemu ya juhudi kubwa za kimataifa.
Soma zaidi: COVID 19 yazidi kuitesa India
Marekani, Ujerumani, Urusi, Uingereza na Ufaransa ni miongoni mwa mataifa yaliyopeleka misaada ya dharura ikiwemo mitungi ya oksijeni, barakoa na dozi za chanjo.
Balozi wa Ujerumani nchini India Walter J. Lindner, alisema baada ya mashine 120 za kusaidia kupumua kuwasili Jumamosi, kuwa wakati mwingine watu wanafariki nje ya hospitali kwa sababu hawana oksijeni na wengine wanafariki wakiwa kwenye magari yao. New Delhi ambayo ni mojawapo ya maeneo yaliyoathirika vibaya kabisa India, ilirefusha kwa wiki moja amri ya kusitisha shughuli za kawaida.
Anthony Fauci, mshauri mkuu wa janga la corona nchini Marekani, amesema India nzima inapaswa kutangaza kufungwa kwa shughuli za kawaida ili kupambana na wimbi hili la corona.
Serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi imesita kutangaza amri ya kusitishwa shughuli za kawaida kote nchini lakini majimbo mengi yametangaza vizuizi vikali.
Soma zaidi: Wimbi la maambukizi ya Covid-19 bado laitikisa India
Nchi kadhaa zimesitisha safari kutoka India, huku Nigeria jana ikipiga marufuku wasafiri wote ambao wamekuwa India kwa wiki mbili zilizopita, ijapokuwa Wanaigeria na wale wanaounganisha safari zao India wataruhusiwa.
Modi apoteza uchaguzi wa mkoa muhimu
Wakati huo huo, chama cha Waziri Mkuu wa India Narendra Modi cha Uazalendo wa Kihindu - Bharatiya Janata - BJP kimepata pigo baada ya kupoteza katika uchaguzi wa mkoa uliokuwa na ushindani mkali wa Bengal Magharibi. Matokeo yanaonyesha kuwa chama cha Trinamool Congress – TMC cha Mamata Banerjee kimeshinda kwa muhula wa tatu.
Soma zaidi: Hali ya maambukizi imekuwa mbaya nchini India
Kwa Zaidi ya mwezi mmoja India iliandaa zoezi lake kubwa kabisa la kidemokrasia katika miaka miwili, huku watu milioni 175 wakiwa wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi wa mikoa mitano. Watalaamu wanasema uzembe kuhusu janga, pamoja na sherehe za kidini zilizohudhuriwa na mamilioni ya waumini na mikutano ya kisiasa, vilichangia kusambaza virusi vya corona.
AFP