1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID 19 yazidi kuitesa India

29 Aprili 2021

Wizara ya afya nchini India imesema taifa hilo la Kusini mwa Asia limerekodi maambukizi mapya zaidi ya laki tatu na nusu ndani ya saa 24 zilizopita na kufikisha idadi jumla ya watu walioambukizwa kufikia milioni 18.3.

https://p.dw.com/p/3sjgO
TABLEAU | Indien Coronavirus
Picha: Idrees Mohammed/Sputnik/dpa/picture alliance

Huku hayo yakiarifikiwa Kenya imeungana na mataifa mengine duniani kusimamisha kwa muda safari za ndege kutoka India kufuatia ongezeko la maambukizi hayo. 

Ikiwa na maambukizi mapya elfu 379,257 India, kwa sasa imeripoti visa zaidi ya milioni 18.3 vya maambukizi ya virusi vya corona ikichukua nafasi ya pili ya taifa lililo na idadi kubwa ya maambukizo baada ya Marekani.

Wizara ya afya pia imeripoti vifo 3,645 ndani ya saa 24 zilizopita na kufikisha idadi jumla ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa wa COVID-19 kufikia elfu 204,832. Kwa siku saba mfululizo India imerekodi maambukizi mapya zaidi ya laki tatu na nusu kila siku hali inayopelekea mfumo wake wa afya kuendelea kulemewa na kusababisha mataifa ya nje kutuma misaada ya haraka.

Kulingana na wataalamu, taifa hilo la Kusini mwa Asia lililo na idadi ya watu bilioni 1.4 halikufikiria kuwa litaelemewa baada ya maambukizi kupungua mwezi Septemba, lakini kutokana na mikusanyiko ya watu wengi, hasa katika mikutano ya kisiasa, sherehe za kidini na watu kutochukua tahadhari ya kujikinga pamoja na matamshi ya viongozi wanaojisifu kuwa India imeshhinda vita dhidi ya virusi hivyo na ndio sababu zinazosemekana kusababisha taifa hilo kukumbwa na makali ya corona. Aina mpya ya kirusi cha corona pia kinasemekana kuchangia ongezeko hilo.

TABLEAU | Indien Coronavirus
Hospitali nyingi zinaarifu zimeelemewa na wagonjwa na kukosa mitungi ya kutosha ya gesi ya Oksijeni Picha: Raj K Raj/Hindustan Times/imago images

Mataifa mengi yazuia safari za ndege kutoka india.

Licha ya hali kuwa mbaya uchaguzi katika jimbo la Bengal umeanza hii leo, wakati makali ya ugonjwa huo yakiendelea kusambaa. Zaidi ya watu milioni 8 wanatarajiwa kushiriki uchaguzi huo huku tume ya uchaguzi ikisema imeweka masharti ya kuzingatiwa ya kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo katika zoezi hilo. Hata hivyo waziri Mkuu Narendra Modi pamoja na chama chake cha Bharatiya Janata wamekosolewa kwa kuandaa mikutano ya hadhara ya kisiasa katika wiki chache zilizopita.

Kuanzia jana Jumatano raia wote wa India walio miaka 18 na zaidi wameruhusiwa kujiandikisha mtandaoni kupokea chanjo dhidi ya virusi vya corona zoezi linalotarajiwa kuanza siku ya Jumamosi. India ambayo ni moja ya watengenezaji mkubwa wa chanjo duniani,  haina chanjo za kutosha za kuwapa watu wake.

Taifa hilo pia halina vitanda vya kutosha vya kuwalazia wagonjwa na mitungi ya gesi ya oksijeni pamoja na vifaa vengine muhimu vya hosipitali. Marekani imesema itatuma vifaa hivyo pamoja na mitungi 1,000 ya hewa hiyo pamoja na barakoa milioni 15 aina ya N95. Uingereza imeshatuma misaada ya dawa nchini humo, huku Ufaransa, Ujerumani, Urusi, Ireland na Australia wakiahidi kulisaidia taifa hilo.

Sikiliza hapa: 

29.04.2021 Matangazo ya Asubuhi

Kwa sasa Marekani imewaomba raia wake wote kuondoka nchini India kufuatia ongezeko kubwa la maambukizi ya corona. Kenya nayo imeungana na mataifa mengine kama Australia, Canada, Malaysia, Ubelgiji na Italia kusimamisha kwa muda safari zake za ndege kwenda nchini India. Kulingana na wizara ya afya ya Kenya, wasafiri watakaoingia nchini Kenya kutoka India ndani ya saa 72 zijazo inabidi wakae karantini kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao nchini humo.