MSF: Watoto 13 hufariki kila siku kwa utapiamlo Darfur
6 Februari 2024Taarifa hii ni kulingana na Shirika la Hisani la Madaktari Wasio na Mipaka-MSF ambalo limesema kuwa hayo ni matokeo ya vita vilivyodumu kwa zaidi ya miezi 10 nchini humo.
Kulingana na Claire Nicolet, mkuu wa kitengo cha dharura cha MSF nchini Sudan, mtoto mmoja hupoteza maisha kila baada ya saa mbili katika kambi hiyo na kwamba wale wenye utapiamlo uliokithiri na ambao bado hawajafa, wako hatarini zaidi kufa ndani ya wiki tatu hadi sita ikiwa hawatapatiwa matibabu.
Shirika la MSF inasema kuwa kambi ya Zamzam ambayo inawapa hifadhi zaidi ya watu 300,000 na ambyo iliundwa kwa ajili ya wale waliokimbia ghasia za kikabila zilizoshuhudiwa eneo hilo mwaka 2003, sasa haipati misaada muhimu ya kibinaadamu na huduma ya matibabu kutokana na vita vilivyoanza Aprili mwaka 2023.
Soma pia: WFP: Sudan hatarini kukumbwa na baa kubwa la njaa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya misaada yaliondoka Kaskazini mwa Darfur mara tu baada ya vita kuanza mwezi Aprili mwaka jana, na tangu wakati huo, uwepo wa mashirika hayo ni mdogo.
MSF imesema kuwa watu wa eneo hilo wametelekezwa na kwamba hakuna usambazaji wa chakula kutoka kwa Mpango wa Chakula Duniani tangu mwezi Mei mwaka 2023. Jambo linalopelekea tatizo uhaba mkubwa wa chakula na watoto kupoteza maisha.
MSF iliahidi kuongeza kwa kasi ya utoaji matibabu katika kambi hiyo hasa kwa watoto walio katika hali mbaya zaidi. Walakini, kiwango cha maafa kinahitaji hatua pana zaidi kuliko zile zinazochukuliwa na MSF pekee.
Mzozo huo ni tishio kwa ongezeko la wakimbizi barani Ulaya
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, Filippo Grandi amesema Ulaya huenda ikalazimika kukabiliana na wimbi jipya la wahamiaji kutoka Sudan ikiwa makubaliano ya kusitisha vita hayatosainiwa hivi karibuni kati ya pande mbili zinazozozana nchini Sudan, pamoja na kuimarishwa juhudi za utoaji msaada.
Grandi amesema nchi za Umoja wa Ulaya mara zote zina wasiwasi kuhusu watu wanaovuka bahari ya Mediterrania kukimbilia barani Ulaya, basi hivi sasa zinapaswa kuwa na tahadhari juu ya uwezekano wa kumiminika wakimbizi kutoka Sudan watakaopitia Libya, Tunisia na bahari ya Mediterrania.
Grandi ameyasema hayo siku moja baada ya kutembelea mataifa ya Sudan na Ethiopia. Zaidi ya watu milioni 9 wanakadiriwa kuachwa bila makaazi ndani ya Sudan na wengine milioni 1.5 wamekimbilia nchi za jirani katika kipindi cha miezi 10 ya vita kati ya jeshi la Sudan linaloongozwa na jenerali Abdel-Fattah al Burhan na kundi la wanamgambo la RSF linaloongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.
Soma pia: Umoja wa Ulaya washutushwa na mauaji ya raia 1,000 Darfur
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, vikosi vya wanamgambo wa Dagalo vimeonekana kujiimarisha huku vikilenga kuyadhibiti maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Sudan. Pande zote mbili katika mzozo huo zimeshutumiwa kwa vitendo vya uhalifu wa kivita.
Washirika wa kikanda barani Afrika wakishirikiana na Marekani na Saudi Arabia wamekuwa wakijaribu kuwapatanisha mahasimu hao, ambapo harakati hizo ziliwezesha duru kadhaa za mazungumzo ambayo hayakufanikiwa. Tangu kuanza kwa mzozo huo, Burhan na Dagalo bado hawajakutana ana kwa ana.
(Chanzo: AP)