1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto wa Museveni azusha mjadala kwa kuiunga mkono Urusi

Lubega Emmanuel2 Machi 2022

Bunge nchini Uganda limeitaka serikali kutoa msimamo wake juu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, baada ya mtoto wa rais Mohoozi Kainerugaba kuweka ujumbe kwenye Twitter akiiunga mkono Urusi na kuzusha mjadala.

https://p.dw.com/p/47sxj
Uganda Kampala | Muhoozi Kainerugaba
Picha: Peter Busomoke/AFP/Getty Images

Hivi karibuni mwanawe rais Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni kamanda wa jeshi la nchi kavu aliandika kwenye ukurasa wake wa tweeter kuwa uvamizi huo ulistahili kwani mataifa ya Magharibi yamelenga kuitumia Ukraine kuichokoza Urusi.

Alilinganisha uvamizi huo na kisa cha Urusi kuweka zana zake nchini Cuba mwaka 1962 ambapo Marekani iliingiwa na wasiwasi na kutisha kuanzisha vita vya tatu vya dunia ikidai kuwa Urusi wakati huo ikiitwa Usovieti ilikuwa inaichokoza.

Ujumbe huo unaodhihirisha kuwa jenerali huyo anaiunga mkono Urusi umeibua mjadala nje na ndani ya bunge la Uganda, watu wakihoji kama ni kielelezo cha msimamo wa serikali ya Uganda.

Uganda | Yoweri Museveni während Interview
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

"Sisi hatujui kama Jenerali Muhoozi aliyatoa hayo kama jenerali au mtu binafsi Si vizuri mtu mmoja kutoa msimamo Tunataka kujua msimamo wa serikali," alisema mbunge wa upinzani ambaye ni rais wa chama Justice Forum, Asumani Basalirwa.

Hii si mara ya kwanza kwa ujumbe wa tweeter kutoka kwa Jenerali Muhoozi kuibua mjadala. Wiki iliyopita alisambaza ujumbe akiyaonya makundi hasimu ya serikali ya Rwanda kutotumia ardhi ya Uganda kuendesha harakati zao dhidi ya utawala wa rais Kagame.

Soma pia: Mwandishi aliyekimbia mateso Uganda awasili Ujerumani

Kwa baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa walionukuliwa na  gazeti la kikanda, ujumbe huo ni kama ulionyesha kuwa Uganda inakiri kuwa madai ya Rwanda ya siku zote ni kweli.

Museveni atakiwa kumdhibiti mwanae

Moja ya wachambuzi mashuhuri wa masuala ya kisiasa nchini Uganda, Nicholas Sengooba, amemshauri rais Museveni kumdhibiti mwanawe asije akailetea Uganda shida.

"Wakati wa mzozo unaposema unaunga mkono upande fulani bila shaka umeonyesha  kuwa upande ule mwingine ni adui," alisema mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa na kimataifa John Kibego.

WM Anschlag Uganda Parlament Flaggen Halbmast Terrorismus
Bunge la Uganda linaitaka serikali ya nchi hiyo kutoa msimamo juu ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ili kuepusha utata kwa raia.Picha: AP

Bunge limeitaka serikali kuwasilisha msimamo wake haraka iwezekanavyo, lakini waziri wa mahusiano ya kimataifa Okello Oryem amesema alichokiandika Muhozi kwenye ukurasa wake wa Twitter ni maoni yake binafsi na siyo msimamo wa serikali.

Soma pia: HRW: Uganda ichunguze ukandamizaji wa wanaharakati

Mahusiano na pia miradi ya kibiashara kati Uganda na Urusi mara nyingi husababisha maswali kadhaa bila majibu.

Kwa mfano kwa sasa wabunge wanataka kampuni ya Urusi iliyopewa kandarasi ya kufuatilia magari kwa kuyapa nambari maalum za kidijitali ifafanue jinsi ilivyopata kandarasi hiyo na pia uwezo wake wa kuitekeleza bila kuingilia maisha binafsi ya watu.