Mwendesha mashtaka kesi ya Bhutto, auawa
3 Mei 2013Chaudhry Zulfikar, ameuawa leo asubuhi kwenye mji mkuu wa Islamabad, wakati akielekea mahakamani. Afisa wa polisi, Shan Mohammed, amesema kuwa Chaudhry Zulfikar ameuawa kwa kupigwa risasi mara 13, baada ya watu wenye silaha kulishambulia gari lake muda mfupi alipoondoka nyumbani kwake mjini Islamabad, wakati akielekea katika mahakama ya kupinga ugaidi mjini Rawalpindi.
Shan amesema kuwa katika shambulio hilo, walinzi wawili wa Zulfikar, wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa afisa huyo wa polisi, Zulfikar, alipigwa risasi kichwani, begani na kifuani, hatua iliyosababisha ashindwe kulidhibiti gari lake ambalo lilimgonga mwanamke mpita njia na kumuuwa.
Afisa mwingine wa polisi, Yasin Farooq, amesema washambuliaji hao walifanikiwa kukimbia mara baada ya kufanya shambulio hilo na kwamba msako mkali umeanza kufanywa ili kuwabaini washambuliaji hao.
Kesi alizokuwa anazichunguza
Zulfikar, amekuwa akichunguza kesi kadhaa muhimu, ikiwemo ya mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Benazir Bhutto, aliyeuawa mwaka 2007, mauaji ambayo kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Pervez Musharraf, anatuhumiwa kuhusika. Mwendesha mashtaka huyo, pia alikuwa anachunguza kesi ya wapiganaji wanaohusishwa na shambulio la kigaidi la mwaka 2008 kwenye mji wa Mumbai, India.
Farooq, amesema sababu za mauaji hayo bado haijajulikana, ingawa inashukiwa kwamba kuhusika kwa Zulfikar katika kesi hizo mbili muhimu, huenda ikawa ni sababu ya kuuawa kwake. Waendesha mashtaka wa serikali wamemtuhumu Musharraf kuhusika kwake katika mauaji ya Bibi Bhutto na kwamba hakutoa ulinzi wa kutosha kwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini Pakistan.
Hata hivyo, Musharraf, ambaye alikuwa madarakani wakati Bhutto anauawa, amekanusha madai hayo. Waendesha mashtaka wamewaambia waandishi wa habari kuwa hivi karibuni Zulfikar alipokea vitisho vya mauaji kutokana na kuhusika kwake na upelelezi wa kesi ya Bhutto, lakini hawajasema vitisho hivyo vilitoka kwa nani na wala vilikuwa vinaelezea nini.
Rais alaani mauaji hayo
Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, ambaye ni mume wa Bibi Bhutto, amelaani vikali mauaji hayo na amewaamuru maafisa wa polisi kuhakikisha wanawakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria waliohusika na mauaji hayo.
Mauaji hayo yamefanyika siku chache kabla Pakistan haijafanya uchaguzi wake mkuu wa kihistoria tarehe 11 ya mwezi huu wa Mei. Taarifa zinaeleza kuwa mwaka uliopita, Zulfikar alipewa ulinzi zaidi na serikali, baada ya jina lake kutajwa katika vitisho vilivyopatikana kwa wapelelezi wa polisi wanaochunguza kesi ya Bhutto.
Zulfikar, alikuwa pia mwendesha mashtaka kiongozi wa serikali katika kesi ya shambulio la kigaidi la mwaka 2008, lililofanyika Mumbai, India na kuwaua watu 166. Kundi la wapiganaji la Lashkar-e-Taiba lenye makao yake Pakistan, linashutumiwa kwa kuhusika na shambulio hilo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,APE,AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman