ICC yatafuta waranti wa kuwamata viongozi wa Israel na Hamas
20 Mei 2024Khan amesema anaamini kwamba Netanyahu, waziri wake wa ulinzi Yoav Gallant na viongozi watatu wa Hamas wanahusika na uhalifu wa kivita pamoja na uhalifu dhidi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza na nchini Israel.
Mwendesha mashtaka mkuu huyo wa ICC ni lazima aombe vibali kutoka kwenye jopo la mwanzo la majaji watatu, ambao huchukua wastani wa miezi miwili kuutathmini ushahidi na hapo ndipo watakapoweza kuamua kama kesi hiyo inaweza kuendelea mbele.
Soma Zaidi: Israel yakosoa kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini ICJ
Karim Khan ameandika kwenye taarifa yake kwamba ana ushahidi wa kutosha dhidi ya watuhumiwa hao watano utakao mwezesha kuwashtaki kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika vita kati ya Israel na Hamas. Amesema viongozi wa Hamas Yehia Sinwar, Mohammed Deif na Ismail Haniyeh wanawajibikia, miongoni mwa mambo mengine, mauaji, utekaji nyara na ubakaji tangu kundi hilo lilipofanyika shambulio la tarehe 7 Oktoba.
Khan amesema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa ulinzi Yoav Gallant wanalaumiwa kwa vifo vya raia katika hatua walizochukua kujibu mashambulizi ya Hamas, ikiwa ni pamoja na kulipua mabomu na njaa kama mbinu katika vita hivyo.
Hata hivyo Israel sio mwanachama wa mahakama ya ICC, na hata kama vibali vya kukamatwa viongozi hao vitatolewa, Netanyahu na Gallant hawatakabiliwa na hatari yoyote ya kufunguliwa mashtaka haraka.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz amesema uamuzi huo wa mwendesha mashtaka mkuu wa ICC ni aibu ya kihistoria ambayo itakumbukwa milele.
Kundi la Hamas katika taarifa yake limeukosoa uamuzi wa Karim Khan wa kutaka kuwakamata viongozi wake kadhaa limesema Khan ameshindwa kutofautisha mwathiriwa na mwenye kufanya maonevu.
Soma Zaidi: Mapigano yanaendelea katika mji wa kusini mwa Gaza Rafah
Wakati huo huo mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Jake Sullivan anaendelea na ziara yake nchini Israel, huku kukiwa na juhudi za kutafuta mafanikio ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza.
Sullivan alikutana na kiongozi wa upinzani wa Israel Yair Lapid. Baadaye alikutana kwenye makao makuu ya jeshi la Israel na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant na Mkuu wa Majeshi Luteni Jenerali Herzi Halevi. Gallant alimwambia Sullivan kwamba Israel itaendeleza mashambulizi yake ya ardhini huko Rafah ili kulisambaratisha kundi la Hamas na kuwakomboa mateka wake.
Baada ya mkutano huo, mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani alikutana na wajumbe wawili wa baraza la mawaziri linalosimamia vita Benny Gantz na Gadi Eisenkot. Haya yanajiri huku Gantz akitishia kukiondoa chama chake cha National Unity kutoka kwenye serikali ya muungano kama Waziri Mkuu Netanyahu hatotangaza mpango unaolezea mkakati mpya.
Vita vya Israel na Hamas
Vita hivyo vilianza na shambulio la kushtukiza la Hamas kusini mwa Israel mwaka jana, ambapo wanamgambo hao waliwaua takriban watu 1,200, na kuwachukua mateka wengine 250.
Wapalestuina wasiopungua 35,000, wameuawa kwenye vita hivyo kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza. Takriban asilimia 80 ya idadi ya Wapalestina milioni 2.3 wameguka kuwa wakimbizi wa ndani wanaohamahama kila mara kutoka eneo moja Kwenda kweye maeneo mengine katika Ukanda wa Gaza.
Vyanzo:RTRE/AFP/AP/DPA