Mwendesha mashtaka Ujerumani aonya juu ya kitisho cha ugaidi
19 Juni 2024Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali Jens Rommel ameeleza kuwa kati ya matukio 700 ya uchunguzi uliofanyika mwaka uliopita kuhusu ugaidi na usalama wa serikali, karibu matukio 500 yalihusishwa na ugaidi unaochochewa na itikadi kali za kidini.
Ameongeza kuwa zaidi ya matukio 40 yalihusiana na uhalifu uliochochewa na siasa kali za mrengo wa kulia na matukio mengine matatu yalichochewa na itikadi kali za mrengo wa kushoto.
Soma pia: Hali ya usalama nchini Ujerumani bado ni tete, majasusi
Kadhalika, idadi ya matukio ya uhalifu yanayochochewa na siasa yameongezeka maradufu.
Mwendesha Mashtaka Mkuu huyo ametolea mfano wa tawi la kundi linalojiita Dola la Kiislamu la Khorasan na jinsi linavyoilenga Ujerumani kwa mashambulizi na kusajili wapiganaji wapya.