Mzozo wa Gaza watishia kutanuka kote Mashariki ya Kati
31 Januari 2024Makundi hayo yanapatikana katika mataifa ya Lebanon, Iraq Yemen na Syria na hufanya mashambulizi dhidi ya mali na maeneo yanayokaliwa na vikosi vya Israel na Marekani.
Hii leo jeshi la Marekani limeeleza kuwa lilinasa na kuharibu kombora lililofyetuliwa na waasi wa Houthi nchini Yemen kuelekea Bahari Nyekundu. Waasi hao wamekuwa wakishambulia meli za biashara zinazopita katika Bahari hiyo ya Shamu wakidai kuwa vitendo hivyo vinalenga kudhihirisha uungwaji wao mkono kwa Wapalestina.
Soma pia: China yaonya dhidi ya kutanuka mzozo wa mashariki ya kati
Kundi la wanamgambo la Kataib Hezbollah la huko nchini Iraq na ambalo linaungwa mkono na Iran, limetangaza kusitisha mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya Marekani ili kuiepusha "matatizo" serikali mjini Baghdad. Wanamgambo hao hata hivyo wamesema wataendeleza mshikamano wao na Wapalestina kwa "njia nyingine" ambazo hazikutajwa.
Siku ya Jumapili, wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa nchini Jordan huku Washington ikiapa kulipiza kisasi. Leo hii Iran imeionya Marekani kwamba itajibu shambulio lolote dhidi yake huku kamanda wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran (IRGC), Hossein Salami, akisisitiza kwamba Iran haitaki vita, lakini pia haiogopi vita.
Mapigano yaendelea katika Ukanda wa Gaza
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema kuwa wanamgambo 25 wa Kipalestina na wanajeshi wake watatu wameuawa huko Gaza katika muda wa masaa 24 yaliyopita.
Kulingana na Jeshi la Israel, wanamgambo 15 wa Hamas wameuawa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na wengine 10 katika eneo la katikati mwa ukanda huo. IDF imesema pia kwamba wanachama 10 wa kundi la Islamic Jihad linaloshirikiana na Hamas, wamekamatwa katika operesheni iliyoilenga shule moja ambayo IDF inadai ilikuwa ikitumiwa kama maficho ya magaidi hao. Aidha jeshi hilo la Ulinzi la Israel limesema limefanikiwa kuharibu roketi tano za magaidi hao.
Soma pia: Makomandoo wa Israel wawauwa Wapalestina watatu hospitalini
Mapigano pia yameendelea kuripotiwa katika mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis, ambapo IDF imesema imeshambulia "maficho ya silaha" na kambi ya kijeshi ya Hamas. Mashuhuda wanasema maeneo makubwa ya jiji hilo yameharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya mabomu ya Israel.
Vikosi vya Israel vinasema vimeanza kuyashambulia pia mahandaki ya Hamas huko Gaza, katika juhudi za "kuzuia tishio la mashambulizi ya chini ya ardhi" ya kundi hilo.
Kwa mujibu wa Wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas, watu 26,900 tayari wameuawa huko Gaza tangu kuanza kwa vita hivyo Oktoba 7 mwaka jana.
Hayo yakiripotiwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor amesema hii leo kuwa mataifa yote duniani yana wajibu wa kusitisha ufadhili kwa jeshi la Israel hasa baada ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, ambayo iliitaka Israel kuchukua hatua zote zilizo ndani ya uwezo wake ili kuwazuia wanajeshi wake kutofanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
(Vyanzo: Mashirika)