1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Namibia yamchagua rais wa kwanza mwanamke

4 Desemba 2024

Namibia imemchagua rais wake wa kwanza mwanamke baada ya chama tawala cha SWAPO kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/4niGP
Rais mteule wa Namibia, Makamu wa Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah
Rais mteule wa Namibia, Makamu wa Rais Netumbo Nandi-NdaitwahPicha: Esther Mbathera/AP Photo/picture alliance

Tume ya Uchaguzi ya Namibia ECN, usiku wa kuamkia Jumatano ilitangaza kuwa Makamu wa Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah, ameshinda kwa zaidi ya asilimia 57 ya kura akifuatiwa katika nafasi ya pili na mgombea wa chama kikuu cha upinzani Patriots for Change IPC, Panduleni Itula aliyepata asilimia 25.5.

Itula na chama chake cha IPC lakini walisema kwamba hawatambui matokeo ya uchaguzi huo ambao wanadai ulikumbwa na udanganyifu mwingi.

Nandi-Ndaitwah mwenye umri wa miaka 72, sasa anakuwa mwanamke wa kwanza kuitawala nchi hiyo ya kusini mwa Afrika iliyo na utajiri wa madini. Namibia imeongozwa na chama cha SWAPO tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1990.

Kusubiri makaratasi ya kura kwa masaa 12

Zoezi la upigaji kura liliongezewa muda kutoka Novemba 27hadi Novemba 30 baada ya matatizo ya kiufundi, ikiwemo uhaba wa makaratasi ya kupigia kura, jambo lililopelekea milolongo mirefu kushuhudiwa.

Makamu wa Rais Netumbo akipiga kura yake
Makamu wa Rais Netumbo akipiga kura yakePicha: Esther Mbathera/AP Photo/picture alliance

Baadhi ya wapiga kura walikata matumaini ya kupiga kura hiyo siku ya kwanza baada ya kusubiri kwa zaidi ya masaa 12. Chama cha IPC kilisema kwamba hii ilikuwa hatua ya makusudi na kwamba hakitokubali matokeo.

Shirika moja la mawakili wa haki za binadamu kusini mwa Afrika lililokuwa linahudumu kama mwangilizi wa uchaguzi huo lilisema pia, hatua hiyo ya uhaba wa karatasi za kura na kucheleweshwa kwa zoezi la upigaji kura hizo lilifanyika kimakusudi na kwamba lilitokea katika maeneo mengi.

Itula mwenye umri wa miaka 67 alisema wiki iliyopita kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na mapungufu mengi. Aliongeza kwamba chama cha IPC kitapambana kwa kutumia njia zote za mchakato wa uchaguzi nchini humo kuhakikisha kwamba zoezi zima la uchaguzi limefutiliwa mbali.

Msemaji wa chama cha IPC Imms Nashinge akizungumza baada ya tangazo la Jumanne kuhusiana na ushindi wa SWAPO, alisema chama hicho kinashikilia msimamo wake wa kutokubali matokeo.

Tume ya Uchaguzi nchini Nambia ECN ilikiri kufeli katika maandalizi ya uchaguzi huo, ikiwemo upungufu wa makaratasi ya kupigia kura na kupata moto kupita kiasi kwa kompyuta zilizokuwa zinatumika kuwasajili wapiga kura.

SWAPO chapata wingi wa bunge pia

ECN ilisema Jumanne, kati ya watu milioni 1.5 waliojiandikisha kupiga kura karibu asilimia 77 walipiga kura zao katika kura ya rais.

Mgombea wa upinzani Dokta Panduleni Itula
Mgombea wa upinzani Namibia Dokta Panduleni Itula (katikati)Picha: Hildegard Titus/AFP/Getty Images

"Raia wenzangu wa Namibia, uchaguzi huwa wenye ushindani kwa kawaida ila demokrasia inatutaka sote tuungane mara yanapotangazwa matokeo. Natoa wito kwa Wanambia wote wayakumbatie matokeo kwa umoja, maelewano na maridhiano," alisema mwenyekiti wa ECN Elsie Nghikembua baada ya kutangaza matokeo hayo yaliyokipa ushindi chama cha SWAPO.

Chama cha SWAPO pia kimepata wingi wa bunge kwa kupata viti 51 ikilinganishwa na 20 vya chama cha IPC.

Namibia ina utajiri mkubwa wa madini ya urani na almasi ila wachambuzi wanasema ni watu wachache katika idadi ya watu milioni tatu raia wa nchi hiyo walionufaika na utajiri huo, katika masuala kama miundo mbinu bora na fursa za ajira.

Ukosefu wa ajira kwa vijana walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 34 unakadiriwa kuwa asilimia 46, hiyo ikiwa ni mara tatu ya wastani wa kitaifa.

Chanzo: AFP/DPA