1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Narendra Modi atoa onyo kali kwa Pakistan

15 Februari 2019

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameionya Pakistan itarajie majibu makali baada ya shambulio la bomu katika eneo la mzozo la Kashmir, tukio lililoanzisha mgogoro kati ya nchi hizo mbili zinazomiliki silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/3DTcX
Narendra Modi
Picha: Getty Images/AFP/M. Sharma

Shambulio hilo la bomu lililotegwa ndani ya gari ya msafara wa kijeshi linasemekana kuwa baya zaidi tangu kuanza kwa mashambulizi ya uasi muongo mmoja uliopita katika maeneo ya Jammu na Kashmir majimbo yanayokaliwa na waislamu wengi nchini humo.

Kufuatia shambulio hilo, Waziri Mkuu Narendra Modi amesema watatoa majibu makali kwa Pakistan na hawatokubali kusambaratishwa na taifa hilo. Modi aliyasema hayo baada ya kukutana na washauri wa usalama.

"Kama nchi jirani ambayo imetengwa na dunia nzima inadhani hatua inayochukua, na mbinu inayotumia zitafanikiwa kuisambaratisha India, basi waache kuota, hawataweza kufanya hivyo na hakuna kitu kama hicho kitawahi kutokea," alisema Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.

Hata hivyo kundi la wanamgambo la Jaish e Mohammed nchini Pakistan lilikiri kuhusika na shambulio hilo punde tu baada ya mshambuliaji wa kutoa muhanga alipolivurumisha gari lililojaa mabomu katika basi lililokuwa limewabeba wanajeshi.

Shambulio hilo limetokea miezi michache kabla ya India kuandaa uchaguzi mkuu.

Pakistan yakanusha kuhusika na shambulio la bomu Kashmir

Indien Selbstmord-Attentat in Kaschmir
Wanajeshi wa India wasimama kando ya basi la wanajeshi lililoshambuliwaPicha: picture-alliance/AP Photo/U. Asif

India kwa miaka mingi imekuwa ikiishutumu Pakistan kuwaunga mkono wanamgambo wanaotaka eneo zima la Kashmir liunganishwe na Pakistan au litangazwe eneo la kujitegemea. India inasema inaushahidi Pakistan imehusika na shambulio la jana.

Kwa upande wake wizara ya mambo ya kigeni ya Pakistan imesema inalaani vitendo vya vurugu mahali kokote duniani na kukanusha kuhusika na shambulio la bomu lililowaua wanajeshi 44.  Taarifa ya wizara hiyo imesema India inaishutumu bila kufanya uchunguzi wa kubaini kama kweli imehusika au la.

Huku Pakistan ikiendelea kukanusha hilo Marekani imeitaka nchi hiyo kuacha kuwaunga mkono na kuwapa hifadhi wanamgambo na makundi mengine yote ya kigaidi yanayotelkeleza shughuli zake kutoka nchini humo. Hata hivyo kumekuwepo na miito mbali mbali ya kulipiza kisasi kupitia mitandao ya kijamii nchini India.

Arun Jaitley moja ya maafisa wa ngazi za juu serikalini amewaambia waandishi habari kuwa India itahakikisha Pakistan imetengwa kabisa.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo