1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Hezbollah aapa kulipa kisasi kwa Israel

Angela Mdungu
20 Septemba 2024

Kiongozi wa wanamgambo wa Hezbollah Hassan Nasrallah ameahidi kulipa kisasi baada ya mashambulizi yaliyofanywa kupitia vifaa vya mawasiliano vya wanamgambo wake na kusababisha milipuko katika maeneo kadhaa ya Lebanon.

https://p.dw.com/p/4ktPL
Hassan Nasrallah, Lebanon
Kiongozi wa Hezbollah, Hassan NasrallahPicha: Hassan Ammar/AP Photo/picture alliance

Hassan Nasrallah wakati wa hotuba yake ya Alhamisi aliapa kulipa kisasi na kuongeza mashambulizi dhidi ya Israel licha ya mashambulizi ya vifaa vya mawasiliano yaliyowalenga wanamgambo wake Juma hili.

Nasrallah amesisitiza kuwa raia wa Israel waliolazimika kuyahama makazi yao karibu na mpaka wa Lebanon kutokana na mapigano, hawatarejea kwenye makazi yao hadi vita kwenye Ukanda wa Gaza vitakapokoma.

Soma zaidi: Hezbollah yailaumu Israel kwa mashambulizi ya kieletroniki Lebanon

Ameyasema hayo huku Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant akieleza kuwa amedhamiria kuwarejesha wakaazi hao makwao.

Galant amesema kuwa, "Lengo letu ni kuhakikisha kuwa jamii za watu wa Kaskazini mwa Israel wanarejea kwenye makazi yao. Kadri muda unavyokwenda, Hezbollah izazidi kulipa gharama kubwa."

Hezbollah inaituhumu Israel kuwa ndiyo iliyohusika na milipuko ya vifaa vyake vya mawasiliano iliyotokea katika maeneo mbalimbali ya Lebanon na Syria. Israel yenyewe haijakanusha wala kukubali kuwa ilihusika.

Shambulio la kielektroniki Lebanon
Moja ya vifaa vya mawasiliano vilivyolipuka LebanonPicha: Balkis Press/ABACA/IMAGO

Soma zaidi: Watu 37 wafariki na maelfu wajeruhiwa kufuatia wimbi la milipuko ya vifaa vya mawasiliano nchini Lebanon

Kuhusu shambulio hilo, Shirika la Usalama la Bulgaria SANS, limesema Ijumaa kuwa hakuna vifaa vya mawasiliano vilivyotumika katika mashambulizi ya Lebanon vilivyotengenezwa, kusafirishwa kuingia, au kuuzwa nje ya Bulgaria.

Katika hatu nyingine, Jeshi la Israel limesema limewashambulia wanamgambo wa Hezbollah saa kadhaa baada ya hotuba ya kiongozi wa kundi hilo aliyeapa kulipa kisasi. Limesema ndege zake za kivita zilishambulia vichwa 100 vya kurusha roketi na silaha zilizokuwa tayari kutumiwa kuishambulia Israel katika siku za usoni.

Walinda amani Lebanon wataka Israel na Hezbollah wapunguze mivutano

Hayo yanajiri huku kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Kusini mwa Lebanon kikitoa wito wa pande zenye mzozo kupunguza mivutano kutokana na ongezeko la mashambulizi katika mpaka wa Israel na Lebanon.

Shambulio la anga katika kijiji cha Khiam Kusini mwa Lebanon
Mashambulizi ya jeshi la anga la Israel dhidi ya LebanonPicha: AFP/Getty Images

 Kwa upande wake Ikulu ya Marekani imesema suluhisho la kidiplomasia linaweza kupatikana katika mzozo huo huku Uingereza ikitoa wito wa kusitishwa haraka kwa mapigano kati ya Hezbollah na Israel.

Wakati hayo yakiendelea, Wahudumu wa afya wanaripoti kuwa Wapalestina 14 wameuwawa leo Ijumaa kutokana na mashambulizi ya anga yanayofanywa na jeshi la Israel Kaskazini na Katikati mwa Ukanda wa Gaza. 

Mashambulizi hayo yamefanywa huku vifaru vya kivita vikielekea Kaskazini Magharibi mwa Rafah, karibu na mpaka wa Misri.