1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yaanza kutoa mafunzo kwa vikosi maalum vya Afghanistan

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssesaanga
29 Julai 2021

Jumuiya ya NATO imezindua mpango wa kwanza wa mafunzo ya nje ya nchi kwa vikosi maalum vya wanajeshi wa Afghanistan. Mafunzo hayo yanafanyika nchini Uturuki

https://p.dw.com/p/3yEzn
Afghanistaneinsatz der Bundeswehr endet
Picha: Torsten Kraatz/Bundeswehr/dpa/picture alliance

Kulingana na habari kutoka mjini Ankara, vikosi maalum vya Afghanistan viliwasili nchini Uturuki hapo jana Jumatano tayari kuanza mafunzo hayo ya kijeshi. Huo ni utangulizi wa mipango ya mafunzo ya kijeshi nje ya Afghanistan.

Msemaji wa jumuiya ya kijeshi ya NATO huko mjini Brussels Oana Lungescu amethibitisha kuanza kwa mafunzo hayo lakini hakutoa maelezo zaidi juu ya eneo halisi yanapofanyiwa mafunzo hayo kwa sababu za kiusalama.

Katibu Mkuu NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu NATO Jens StoltenbergPicha: Torstein/NTB/AP/picture alliance

Msemaji huyo wa NATO amesema pamoja na kuendelea kuipa ufadhili nchi ya Afghanistan na uwepo wa ofisi za kidiplomasia nchini humo, jumuiya ya hiyo ya kijeshi itaendelea kuisaidia Afghanistan katika mpango wa mafunzo ya nje ya kijeshi kwa vikosi maalum vya Afghanistan. Msingi wa kutolewa msaada huo unaoendelea wa jumuiya ya NATO kwa vikosi vya serikali ya Afghanistan ni uamuzi wa wakuu wa nchi na serikali 30 washirika wa jumuiya hiyo ya kijeshi.

Uamuzi huo ulifikiwa kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya ya kijeshi ya NATO mnamo mwezi Juni kwamba wangeendelea kutoa msaada kwa Afghanistan hata baada ya kumalizika kwa ujumbe wa kijeshi nchini humo. Mwisho wa ujumbe wa majeshi ya NATO huko nchini Afghanistan uliamuliwa hapo mwezi Aprili baada ya Marekani, iliyokuwa na kikosi kikubwa cha jeshi nchini Afghanistan ilipoamua kuwaondoa wanajeshi wake kutoka nchini humo.

Soma zaidi:Wanamgambo wa Taliban wakamata miji zaidi Afghanistan

Wakati huo huo Uturuki imejitolea kuulinda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamid Karzai mjini Kabul baada ya vikosi vya Marekani kuondoka hatua ambayo wataalamu wanaiona ni kama jitihada ya Uturuki kutaka kuboresha uhusiano uliovurugika kati yake na Marekani. Uwanja huo wa ndege wa kimataifa ndio salama kwa wafanyikazi wa balozi mbalimbali na unatumika pia kupokea misaada kwa ajili ya nchi ya Afghanistan iliyokumbwa na vita.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Murat Cetinmuhurdar/PPO via REUTERS

Uturuki imesema kuuweka uwanja huo wa kimataifa katika hali salama ni jambo la kupewa kipaumbele kutokana na vikosi vya wapiganaji wa Taliban vinavyozidi kusonga mbele hasa baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kusitisha ushiriki wa nchi yake nchini Afghanistan ambapo wanajeshi wake wataondoka baada ya kuwemo nchini humo kwa muda wa miaka 20. Biden ameagiza wanajeshi wake wote kuwa wameondoka kutoka nchini Afghanistan ifikapo mwisho wa mwezi ujao.

Vyanzo:DPA/AFP