1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yajitayarisha kupambana na kitisho cha Urusi Ukraine

17 Februari 2022

Waziri wa ulinzi wa Uingereza Ben Wallace amesema Jumuiya ya kujihami NATO itaendelea kuimarisha jeshi lake kujiandaa kukabiliana na kitisho cha Urusi.

https://p.dw.com/p/47ALb
UK Politiker Ben Wallace
Picha: Matt Crossick/PA/imago images

Akizungumza kabla ya mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya kujihami NATO na wenzao kutoka Ukraine na Georgia, Waziri Ben Wallace amesema wanafikiria namna watakavyokabiliana na kitisho cha Urusi nchini Ukraine na usalama wa eneo zima akisema suala hili ni changamoto kubwa kwa uthabiti wa Ulaya. 

Waziri huyo wa Ulinzi wa Uingereza amesema njia moja ya kuhahakisha hakuna utanuzi wa migogoro ya kikanda ni kutoa ushirikiano kwa washirika wao wa NATO na hicho ndicho wanachokifanya.

Muungano wa jeshi la Magharibi jana Jumatano lilitoa wito kwa makamanda wake wa kijeshi, kuazisha mipango ya kutuma wanajeshi zaidi kwa wanachama wake wa Mashariki kutokana na kitisho cha uvamizi kutoka Urusi.

Wallace amerejelea madai yake kwamba Urusi inaendelea kupeleka wanajeshi zaidi kati ya mpaka wake na Ukarine licha ya kutangaza hapo jana kwamba inaondoa wanajeshi hao katika eneo hilo. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ameunga mkono tamko la Wallace na kusema mataifa ya Magharibi hajaona dalili yoyote kwamba Urusi inaondoa wanajeshi wake.

OSCE yaripoti matukio ya mashambulizi Mashariki mwa Ukraine

Ukraine | Militärübung
Picha: Vadim Ghirda/AP Photo/picture alliance

Kutokana na hilo wanachama wa NATO wameanza kupeleka wanajeshi wake katika maeneo ya Mashariki. Tayari Marekani imesema inapeleka wanajeshi wake wengine 4,700 nchini Poland huku Wallace akisema Uingereza imeweka wanajeshi 1000 tayari kukabiliana na hatua yoyote ile.

Huku hayo yakiarifiwa waangalizi wa shirika la usalama na ushirikiano barani ulaya OSCE wamerekodi mashambulizi ya makombora katika eneo linalokaliwa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi na wanajeshi wa serikali Mashariki mwa Ukraine.

Watu hao wanaotaka kujitenga awali walisema kwamba vikosi vya serikali viliwashambulia hatua inayozidisha mvutano kuelekea mzozo kati ya Urusi na Mataifa ya Magharibi. Ukraine imekanusha kuwashambulia na badala yake imesema watu hao wanaotaka kujitenga ndio waliotumia makombora dhidi ya wanajeshi wake.

Chanzo: afp/reuters