Netanyahu asitisha mpango tata wa mageuzi ya mahakama
28 Machi 2023Netanyahu ameyatoa matamshi hayo Jumatatu usiku mjini Jerusalem, na kusema kwamba ameamua kusitisha mpango wa kuwasilisha na kuyasoma mapendekezo yake kwa mara ya pili na ya tatu katika kikao cha bunge, hivyo muswada huo hautapelekwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura hadi mwishoni mwa mwezi Aprili. Kwa mujibu wa Netanyahu, wako katikati ya mzozo ambao unatishia umoja wao, hivyo kila mtu anapaswa kuchukua hatua kwa kuwajibika.
Netanyahu aonya kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe
Pia ameonya kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo havipaswi kutokea. ''Iwapo kuna uwezakano wa kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe kupitia mazungumzo, mimi, kama waziri mkuu, nimeamua kufuata njia ya mazungumzo. Ninatoa fursa hii kuhakikisha tunafanya mazungumzo ya kweli na yanayofaa,'' Netanyahu.
Mapema Jumatatu, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel, Itamar Ben-Gvir alisema kuwa yeye pamoja na Netanyahu wamekubaliana kuahirisha mageuzi hayo. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, Ben-Gvir na Netanyahu walikutana kabla, kwa ajili ya kikao cha dharura ambacho inasemekana Ben-Gvir alitishia kujiuzulu iwapo Netanyahu asingezingatia mipango ya mageuzi.
Rais wa Israel, Isaac Herzog ameipongeza hatua ya kusitishwa kwa mpango wa mageuzi, akisema sasa ni muda wa kuanza mazungumzo ya dhati na yenye uwajibikaji ambayo yatapunguza mivutano iliyopo. Herzog ametoa wito kwa pande zote kuwajibika ipasavyo, na kwamba wote wabakie wamoja na kuwa taifa moja la Wayahudi na lenye kufuata demokrasia.
Makundi ya kisiasa yaanza juhudi za mazungumzo
Wakati huo huo, makundi ya kisiasa yanayompinga Netanyahu leo yameanza kuandaa timu zitakazoshiriki kwenye mazungumzo, baada ya Netanyahu kusitisha mpango wake wa mageuzi katika mfumo wa mahakama.
Kiongozi wa upinzani, Yair Lapid amesema wako tayari kuanza mazungumzo ya kweli katika makaazi ya rais, iwapo kweli mpango wa mageuzi ya kisheria utasitishwa. Lapid pia ameonesha mashaka juu ya umakini wa Netanyahu, akisema wamekuwa na uzoefu mbaya huko nyuma, hivyo watahakikisha kwamba hakuna hila wala upotoshaji.
Waziri wa zamani wa ulinzi wa Israel, Benny Gantz amesema ataanza kufanya mazungumzo kwa moyo mmoja. Kulingana na vyombo vya habari, tayari Netanyahu amefanya mazungumzo na Gantz Jumatatu usiku. Inaelezwa kuwa Gantz alimtaka Netanyahu kubatilisha uamuzi wake wa kumfukuza kazi Waziri wa Ulinzi, Yoav Gallant ambaye aliipinga hadharani mipango ya serikali.
Marekani yapongeza hatua ya Netanyahu
Hatua ya Netanyahu imepongezwa pia na Mjumbe wa Marekani nchini Israel, Tom Nides, ambaye amesema waziri huyo mkuu atapewa mwaliko wa kumtembelea Rais Joe Biden mjini Washington hivi karibuni. Kauli hiyo ameitoa Jumanne katika kituo cha redio ya jeshi ya Israel.
Hata hivyo, licha ya kufikiwa kwa hatua hiyo, watu wanaoandaa maandamano kupinga mageuzi hayo ya mfumo wa mahakama ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki kadhaa, wametangaza kuendelea kwa maandamano.
(AP, AFP, DPA)