Netanyahu ataacha urathi gani baada ya vita vya Gaza?
21 Agosti 2024Iwe kwa uzuri au ubaya, ni watu wachache mno ambao majina yao yatakumbukwa zaidi katika muktadha wa vita hivi vya Gaza kuliko Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Shambulio la Oktoba 7 la Hamas, liligharimu maisha ya Waisraeli wapatao 1,200 huku watu zaidi ya 200 wakichukuliwa mateka na kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina lililoorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa mengine ya Magharibi.
Vita vilivyofuata vimekuwa na athari kubwa kwa maisha ya watu katika eneo hilo kwa karibu mwaka mmoja sasa. Wakati huo huo, Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas huko Gaza imesema zaidi ya Wapalestina 40,100 wameuawa hadi sasa.
Kura za maoni zinaonyesha kuwa Netanyahu bado ana uungwaji mkono ulio imara
Kwa ujumla, maoni ya Waisraeli kuhusu Netanyahu yamekuwa yakibadilika kila wakati kutokana na mzozo huo. Kulingana na kura ya maoni ya mwezi Agosti iliyofanywa na jarida la kila siku la Maariv, chama cha Netanyahu cha Likud lingepata ushindi katika majimbo 22 iwapo uchaguzi ungefanyika sasa, na kukifanya kuwa chama kikubwa zaidi nchini Israel, na kukipiku chama cha State Camp cha Benny Gantz.
Soma pia: Maandamano ya kumtaka Benjamin Netanyahu ajiuzulu yafanyika Tel Aviv
Aidha, kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 7 mwaka jana, idadi kubwa ya watu wanafikiri kuwa Netanyahu anafaa zaidi kushikilia wadhifa wa waziri mkuu kuliko Gantz (42% dhidi ya 40%). Gantz, alikuwa mkuu wa zamani wa jeshi na alikuwa sehemu ya baraza la vita la Netanyahu kabla ya kujiuzulu mwezi Juni kutokana na kupingana na maamuzi ya Netanyahu kuhusu vita vya Gaza. Miezi michache tu iliyopita, kura za maoni zilitoa picha tofauti, huku Netanyahu akiwa katika nafasi mbaya.
Netanyahu katika msuguano na familia za mateka
Moja ya masuala makubwa ambayo Netanyahu amekuwa akikabiliana nayo ni mzozo na familia nyingi za mateka wa Israel. Mmoja wa wakosoaji wake wakubwa katika miezi ya hivi karibuni ni Einav Zangauker, mama ambaye mtoto wake Matan ameshikiliwa mateka na Hamas huko Gaza kwa muda wa miezi 10.
Mwanamke huyo amesema kabla ya vita alikuwa akimuunga mkono Netanyahu lakini anavyoshughulikia mchakato wa mazungumzo ya kuachiliwa kwa mateka umemfanya abadili msimamo wake kutokana na kile ambacho waIsrael wengi wanaamini kwamba Netanyahu amekuwa akijaribu kukwamisha makubaliano hayo. Bi Zangauker alinukuliwa na chombo cha habari cha Israel Ynet akisema kuwa Netanyahu ndiye waziri mkuu katili na mwongo zaidi katika historia ya Israel.
Soma pia: Madai ya Israel kukwamisha mazungumzo ya kusitisha mapigano
Maafisa waandamizi wa timu ya mazungumzo ya Israel waliripotiwa kuunga mkono kauli kama hiyo linapokuja suala la majadiliano. Kulingana na vyanzo vya usalama vilivyonukuliwa na kituo cha televisheni cha N12, ni kwamba Netanyahu hataki makubaliano yoyote kwa wakati huu na pia ni kama amekwisha watelekeza mateka.
Netanyahu anakabiliwa pia na changamoto ndani ya serikali yake hasa linapokuja suala la mazungumzo na Hamas. Waziri wa Ulinzi Yoav Galant amekuwa mara kadhaa akiunga mkono maoni yaliyotolewa na mamlaka ya usalama ya Israel inayopendekeza kufikiwa haraka iwezekanavyo kwa mpango huo wa usitishwaji mapigano katika vita vya Gaza.
(DW)