Israel hataridhia makubaliano ya kusitisha vita Gaza
1 Februari 2024Waziri huyo mkuu wa Israel amesema juhudi za kusaka njia ya mateka kuachiliwa huru zinaendelea lakini hatalipa gharama yoyote kufikiwa makubaliano hayo.
Netanyahu aliyasema hayo wakati Qatar, Misri na Marekani zilipokuwa zikiendeleza mazungumzo yaliyokusudiwa kufikia makubaliano kati ya Israel na Hamas ambayo yanaweza kuwakomboa takriban mateka 100 wanaoendelea kushiliwa na Hamas na kuanzisha usitishaji mapigano kwa muda huko Gaza.
Aliendelea kusisitiza kuwa wanafanya kazi wakati wote kuwakomboa mateka wao, kufikia malengo mengine ya vita, ikiwemo kuiangamiza Hamas na kuhakikisha kwamba Gaza haitakuwa tishio tena kwa Israel.
Soma pia:Mzozo wa Gaza watishia kutanuka kote Mashariki ya Kati
Alisema kwa sasa wanafanyia kazi mfumo wa ziada wa kuachiliwa kwa mateka wa Israel, lakini si kwa gharama yoyote.
"Nina mistari mwekundu, hatutamaliza vita, hatutaondoa wanajeshi wetu kutoka Ukanda wa Gaza na sisi hatutawaachilia huru maelfu ya magaidi." Netanyahu alisisitiza katika video.
Kulingana na shirika la habari la Channel 12 ya Israel, mnamo Jumatatu, mkuu wa idara ya Ujasusi ya Israel Mossad, David Barnea, aliwaarifu mawaziri wa baraza la Vita kuhusu vipengee vikuu vya uwezekano wa kuafikia makubaliano.
Ni pamoja na masharti ya mateka 35 wanawake miongoni mwao wakiwa wagonjwa, waliojeruhiwa na wakongwe kuachiliwa huru katika awamu ya kwanza ambapo vita vitasitishwa kwa wiki tano.
Hiyo itafuatwa na usitishaji vita zaidi kwa wiki moja, huku wapatanishi wakijaribu juhudi za kufanikisha mateka vijana na barobaro ambao Hamas huwataja kuwa wanajeshi kuachiliwa huru.
Majadiliano ya Paris yapo matumaini?
Gazeti la Washington Post la Marekani liliripoti kwamba kulingana na rasimu ya makubaliano hayo yanayojadiliwa Paris, raia wote waliokamatwa mateka na Israel wataachiliwa huru katika wiki sita za usitishaji vita endapo, makubaliano yatafikiwa.
Kulingana na ripoti hiyo, wafungwa watatu wa Palestina miongoni mwa maelfu walioko katika magereza ya Israel wataachiliwa huru kwa kila mateka mmoja wa Israel.
Lakini Washington Post ilisema haikuwa wazi ni wafungwa wepi watakaoachiliwa huru na ni nani atakayeamua nani wa kuachiliwa huru.
Soma pia:Vikosi vya Israel vyaendelea kuishambulia Gaza, Hamas yachunguza pendekezo la kusitisha mapigano
Hadi jana, Hamas, kundi la wanamgambo kutoka Palestina, halikuwa limetoa kauli yoyote kuhusu rasimu hiyo ya usitishaji vita. Hayo ni kulingana na gazeti la Times la Israel.
Kundi la Hamas ambalo Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine zimeliorodhesha kuwa la kigaidi, lilifanya shambulizi baya kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7 kando na kuua zaidi ya watu 1,200 walikamata wengine 240 mateka.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya mateka 130 wangali wanashikiliwa Gaza.
Wakati wa makubaliano ya kwanza, zaidi ya mateka 100 waliachiliwa huru mwishoni mwa mwezi Novemba.