Nigeria yagubikwa na mashambulizi kuelekea uchaguzi wa rais
21 Februari 2023Zaidi ya wapigakura milioni 90 wameandikishwa kushiriki kura ya Jumamosi kumchagua mrithi wa rais Muhammadu Buhari ambaye atakuwa anamaliza mihula miwili madarakani. Kuelekea kura hiyo, nchi hiyo inakabiliwa na vitisho tofauti vya kiusalama ikiwa ni pamoja na chachu ya wale wanaotaka kujitenga katika eneo la kusini mashariki lakini pia wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali katika eneo la Kaskazini Mashariki, pamoja na magenge ya utekaji upande wa Kaskazini Magharibi.Nigeria yasema uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa
Msemaji wa polisi Ikenga Tochukwu amesema washukiwa wanaotaka kujitenga walivamia kituo cha polisi cha Awada siku ya Jumatatu kwa kutumia vilipuzi na bunduki. Siku ya Jumapili, polisi wanadai kuwa pia walizuia shambulio jingine kwenye kituo cha polisi cha Nkwelle-Ezunaka na siku moja iliyopita, washambuliaji walikuwa tayari wamevamia kituo cha polisi katika eneo la Ogidi na kuwaua polisi watatu.
Polisi wanalishutumu kundi lililopigwa marufuku la watu wa asili wa Biafra IPOB sambamba na tawi lake lenye silaha la mtandao wa usalama wa Mashariki ESN kwa kufanya mashambulizi ya mara kwa mara, madai ambayo wanakanusha.
Siku ya Jumatatu pia kulishuhudiwa ghasia nyingine katika jimbo la Ogun ambako waandamanaji walichoma moto benki mbili katikati mwa uhaba wa pesa taslimu za Naira. Gazeti la Punch limenukuliwa likisema kwamba ghasia hizo zilizuka kwenye mji wa Sagamu baada ya mashine za benki za kutolea fedha ATM kushindwa kutoa pesa taslimu.Nigeria yaweka kikomo cha utoaji pesa zilizopo benki
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha wakaazi wakishuhudia wateja waliojawa na hasira wakichoma moto benki. Polisi wanadai kuwa wamewakamata watu 27 kuhusu matukio hayo na kwamba hali ya utulivu imerejea. Nigeria inakabiliwa na mgogoro wa uhaba wa noti za Naira wakati serikali ikishinikiza matumizi ya noti mpya kwenye bili ambazo zimechapishwa kabla ya uchaguzi wa Jumamosi.
Vijana ambao ni wapigakura wa mara ya kwanza wana shauku ya kushiriki uchaguzi wa rais wakiwa na matumaini kwamba viongozi wapya wataboresha maisha katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta. Samuel Oludare ni kijana anayetarajiwa kushiriki zoezi hilo na anasema kwamba ''ninaamini kura yangu itakuwa na umuhimu, lakini pia nina hofu kunaweza kuwa na wizi wa kura unaofanywa na watu ambao wanahisi hawawezi kushinda na watafanya mbinu zote muhimu za kuvuruga uchaguzi.''
Mkuu wa jeshi la Nigeria Jenerali Lucky Irabor alisema baada ya kukutana na wakuu wa usalama siku ya Jumatatu kwamba vyombo vya usalama vya nchi hiyo viko tayari kwa uchaguzi. Mfumuko wa bei uliofikia tarakimu mbili, ukuaji hafifu wa uchumi, uhaba wa mafuta na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama ni masuala makubwa yatakayo wasukuma wapigakura katika uchaguzi wa Jumamosi. Mfumuko wa bei sasa umefikia asilimia 21.8, na kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana sasa ni asilimia 43.