Olaf Scholz aidhinishwa kuwa Kansela wa Ujerumani
8 Desemba 2021Rais wa Bunge Bärbel Bas alitangaza rasmi matokeo hayo ya kura ya siri iliyopigwa bungeni leo kumuidhinisha Scholz kuwa kansela mpya wa Ujerumani. Scholz, aliyekuwa naibu kansela na Waziri wa fedha katika serikali ya muungano ameidhinishwa kwa kura 395 katika bunge lenye viti 736 kuchukua nafasi hiyo ya juu katika siasa ya ujerumani.
Chama chake cha SPD na washirika wake wawili, chama cha walinzi wa mazingira Die Grüne au chama cha kijani na kile cha FDP wana takriban viti 416 katika bunge jipya la Ujerumani hali iliyotoa ishara ya mapema kwamba angelishinda nafasi hiyo ya kuwa kansela.
soma zaidi: Scholz ateua Baraza Jipya la Mawaziri Ujerumani
Baada ya kuidhinishwa, Sholz na Baraza lake la mawaziri lililo na wanachama 16, saba kutoka chama cha SPD watano kutoka chama cha kijani na wanne kutoka chama cha FDP wanatarajiwa kuthibitishwa na rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier kabla ya kuapishwa bungeni.
Baadaye mawaziri waliohudumu katika serikali ya Merkel pia watapewa nafasi hii leo kukabidhi madaraka kwa mawaziri wapya. Scholz, aliyehudumu kama waziri wa fedha atamkabidhi majukumu hayo ya kifedha kiongozi wa FDP Christian Lindner.
Mapambano dhidi ya COVID 19 ni moja ya changamoto ya serikali ya Ujerumani
Serikali ya Scholz inaingia madarakani ikiwa na matumaini makubwa ya kuifanya Ujerumani kuwa ya kisasa zaidi kwa kukumbatia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi huku ikikumbwa na chamgamoto kubwa zaidi ya kukabiliana na janga la COVID 19.
Scholz aliye na miaka 63 analeta tajriba kubwa ya uongozi na nidhamu katika serikali yake ya muungano wa vyama vitatu. Ushirikiano wa vyama hivyo unatoa matumaini ya nguvu mpya Ujerumani baada ya miaka 16 ya uongozi wa Angela Merkel.
soma zaidi: Vyama vya Ujerumani vyafikia makubaliano ya kuunda serikali mpya
Serikali mpya ya Ujerumani ina nia ya kuongeza mikakati mipya ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupunguza gesi chafu ya kaboni ikijumuisha kuifanya Ujerumani kutumia kikamilifu nishati endelevu.
Merkel anaondoka madarakani kama kansela wa pili aliyehudumu kwa muda unaofika miaka 16. Mwingine ni Helmut Kohl aliyehudumu kama kansela wa Ujerumani kwa miaka 16 na siku 26 kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 1998.
Chanzo: ap/afp/