1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Mahasimu Sudan tayari kwa mazungumzo ya amani

Sylvia Mwehozi
19 Septemba 2024

Jeshi la Sudan na kikosi kilichoasi cha RSF, yamesema kuwa yako tayari kwa mazungumzo ya amani na kuvimaliza vita ambavyo vinaendelea kwa zaidi ya miezi 17.

https://p.dw.com/p/4kpQw
Abdul Fattah Al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na kiongozi wa kundi la RSF Mohamed Hamdan DagaPicha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan alisema siku ya Jumatano kwamba serikali ya nchi hiyo iko tayari kwa juhudi zote zinazolenga kumaliza vita na wako "tayari kufanya kazi na washirika wote wa kimataifa katika kutafuta suluhu ya mzozo ili kupunguza mateso ya raia na kuiweka Sudan kwenye njia ya kuelekea usalama, utulivu, utawala wa sheria na kupokezana madaraka kwa njia ya kidemokrasia". Hayo ni baada ya wito wa Rais Joe Biden wa kuzitaka pande zote kurejea katika meza ya mazungumzo ya kusitisha mzozo.

Mapema leo kiongozi wa kundi la RSF Mohamed Hamdan Dagalo naye alifuata mwelekeo huo, akisema kuwa wanathibitisha kujitolea kwao katika mazungumzo ya kusitisha vita na wanaamini kwamba amani itapatikana kwa njia ya mazugumzo na sio vurugu. "Tutaendelea kushiriki katika michakato ya amani ili kuwa na mustakabali usio na hofu na mateso kwa raia wote wa Sudan".

Kambi ya wakimbizi wa Sudan nchini Ethiopia
Kambi ya wakimbizi wa Sudan nchini EthiopiaPicha: UNCHCR

EL-FASHER : Waasi wa Dafur wasusia mazungumzo

Hata hivyo makamanda wote wawili hawakutoa mikakati mahsusi kuelekea upatikanaji wa suluhisho la amani. Badala yake wametupiana lawama kwa kushindwa kumaliza mzozo huo ambao umeua zaidi ya watu 12,000 tangu ulipozuka mwaka 2023 na kushutumiana kwa ukandamizaji. 

Wapatanishi wanaoongozwa na Marekani walisema mwezi uliopita kwamba wamepata hakikisho kutoka pande zote mbili katika mazungumzo yaliyofanyika Uswisi kwa ajili ya kuboresha usambazaji wa misaada ya kiutu, lakini kukosekana kwa wawakilishi wa jeshi la Sudan kulidhoofisha mazungumzo hayo kupiga hatua.

Hayo yakijiri, maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa wameonya kwamba maelfu ya maisha ya watu yako hatarini katika mji uliozingirwa wa El-Fashernchini Sudan, katikati mwa hofu kwamba mapigano yanaweza kuongezeka. Umoja wa Mataifa unasema vita katika sehemu kubwa ya Sudan vimesababisha mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani, huku mamilioni ya watu wakikimbia na kusababisha njaa katika kambi ya wakimbizi karibu na El-Fasher. Msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kanda ya Afrika Martha Pobee alilieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa.

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

"Wakati ghasia zikiongezeka huko El Fasher na kuendelea kuenea nchini Sudani, hatari ya ukatili inaongezeka ikiwa ni pamoja na ukatili mkubwa dhidi ya wanawake. Majeshi yote ya RSF na lile la serikali SAF na makundi washirika wao na wanamgambo wanaendelea kutozingatia kabisa haki za binadamu za kimataifa na sheria za kibinadamu."Hujuma za RSF zasababisha kufungwa hospitali muhimu Sudan

El-Fasher ni mojawapo ya miji mikuu katika majimbo matano ya mkoa wa Darfur magharibi mwa Sudan ambao bado haujakamatwa na vikosi vya wanamgambo wa RSF. Takriban watu milioni 1.7 katika eneo la kaskazini la Darfur wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.