1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande hasimu zatenda uhalifu wa kivita Sudan - UN

23 Februari 2024

Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa inasema pande zote mbili kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan zinahusika na matendo ya kikatili yanayoweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/4cnff
Wakimbizi wa Sudan wakiwa kwenye kambi moja nchini Sudan Kusini.
Wakimbizi wa Sudan wakiwa kwenye kambi moja nchini Sudan Kusini.Picha: LUIS TATO/AFP

Wakati juhudi za kukomesha vita hivyo vya miezi kumi sasa zikionekana kugonga mwamba, Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva inasema maelfu ya raia wameshauwa nchini Sudan, maelfu ya wengine wamejeruhiwa na zaidi ya milioni sita wameyakimbia makaazi yao na kuifanya nchi hiyo kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa kabisa ya wakimbizi wa ndani ulimwenguni.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo iliyopewa jina la "Bunduki lazima ziache kutumika na raia lazima walindwe" siku ya Ijumaa (Februari 23) Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amesema ni wazi kuwa baadhi ya matendo haya yanaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.

Soma zaidi: MSF: Watoto 13 hufariki kila siku kwa utapiamlo Darfur

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inaangazia kipindi cha baina ya mwezi Aprili na Disemba mwaka jana na imetokana na mahojiano waliyofanyiwa zaidi ya waathirika na mashahidi 300 pamoja na picha za video na satalaiti. 

Wakimbizi wa Sudan katika kambi moja nchini Sudan Kusini.
Wakimbizi wa Sudan katika kambi moja nchini Sudan Kusini.Picha: LUIS TATO/AFP

Mauaji ya makusudi Darfur

Ripoti inasema kwenye baadhi ya matukio, watu waliokuwa wakikimbia kuyanusuru maisha yao ama wale waliogeuzwa wakimbizi kutokana na mapigano, walikuja kuwa waathirika wa mashambulizi ya makusudi yaliyofanywa na vikosi vya jeshi au vya waasi.

Katika tukio moja, watu zaidi ya kumi waliuawa wakiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Zalingei, jimboni Darfur, baada ya kushambuliwa na vikosi vya RFS baina ya tarehe 14 na 17 Septemba.

Raia wengine 26, wengi wao wanawake na watoto, waliuawa siku ya tarehe 22 Agosti wakiwa wamejificha chini ya daraja kwa makombora yaliyorushwa na jeshi la Sudan.

Wakimbizi wakongwe na changamoto zao

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa wahofia mzozo wa Sudan kuongeza wakimbizi

Ripoti hiyo pia inasema kwamba wapiganaji wa RSF walikuwa wanatumia mbinu ya kijeshi ya kuwatumia raia kama ngao, ikitaja ushuhuda uliotolewa na waathirika wenyewe.

Mauaji ya watoto, wanawake Khartoum

Ripoti inaelezea matukio kwenye mji mkuu, Khartoum, ambako watu kadhaa walikamatwa na kuwekwa nje ya vituo vya RSF ili kukwepa mashambulizi ya ndege za jeshi la Sudan. 

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wameorodhesha visa 118 vya mashambulizi ya kingono, mojawapo ikiwa ya mwanamke mmoja aliyebakwa na kundi zima la wanajeshi kwa wiki kadhaa. Mingi kati ya mikasa hiyo inawahusisha wapiganaji wa kikosi cha RSF.

Wakimbizi wa Sudan wakielekea Sudan Kusini.
Wakimbizi wa Sudan wakielekea Sudan Kusini.Picha: LUIS TATO/AFP

Soma zaidi: Sudan: Makubaliano ya usitishwaji mapigano kufikia tamati

Tayari, Marekani imeshaamuwa rasmi kuwa pande hasimu zinazopigana nchini Sudan zimefanya uhalifu wa kivita, huku ikiwashutumu wapiganaji wa Kikosi cha Dharura chini ya Jenerali Hamdan Dagalo kushirikiana na makundi yenye silaha kuendesha kampeni ya kuwaangamiza raia wa makabila mengine Darfur Magharibi. 

Pande zote mbili, wa RSF na ule wa jeshi la Sudan unaoongozwa na Jenerali Abdel-Fattah Burhani, zimesema zitachunguza ripoti za mauaji na ukatili mwengine na kuwachukulia hatua wapiganaji wao watakaotiwa hatiani kutenda uhalifu huo.

 Reuters