1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa Katoliki: Hakuna tena siri za kashfa za kingono

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
18 Desemba 2019

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ameuondoa mfuniko uliokuwa unafunika siri juu ya kashfa za udhalilishaii wa kingono kwa kufuta kanuni inayozuia kufichuliwa na kuchunguzwa kwa uhalifu huo.

https://p.dw.com/p/3V0Et
Rom Vatikan Eröffnung Amazonas-Synode
Picha: Imago Images/Independent/Catholic Press/M. Migliorato

Papa Francis amechukua hatua hiyo kutokana na kuongezeka kwa malalamiko kwamba kanuni hiyo ilikuwa inatumika kwa ajili ya kuwalinda wahalifu na kuwanyamazisha waliofanyiwa uhalifu wa kingono na pia ilitumika kuwazuia polisi kuchunguza uhalifu.

Watu waliotendewa uhalifu pamoja na mawakili wao wameushangilia uamuzi wa Papa Francis na kwa mtazamo wao, hatua hiyo ilipaswa kuchukuliwa mapema zaidi. Hata hivyo wametahadharisha kwa kusema kwamba ufanisi wa hatua hiyo utathibitishwa pale ambapo kanisa litakapolazimishwa kukubali uchunguzi ufanyike katika nchi husika na nyaraka zote juu ya wahalifu zitolewe hadharani. Juan Carlos Cruz aliyekuwa mhanga wa udhalilishaji wa kiongono kutoka Chile, ambaye sasa ni wakili amesema tamasha la siri sasa limezimwa.

Kwa mujibu wa sheria mpya Papa Francis  ameeleza kuwa habari zinazohusu uhalifu wa kingono zitalindwa  na viongozi wa kanisa lakini ameeleza wazi kwamba kanuni ya kanisa kuficha siri haitatumika tena.

Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini VaticanPicha: picture-alliance/N. Clark

Mchunguzi maarufu wa uhalifu wa kingono Askofu Mkuu Charles Scicluna amesema sheria hiyo mpya ni  hatua muhimu ya kihistoria itakayorahisisha uratibishaji wa sheria na kufungua njia za mawasiliano na watu  waliofanyiwa uhalifu wa kingono.

Mageuzi hayo mapya yalizinduliwa jana Jumanne  ambapo Baba Mtakatifu alitimiza umri wa miaka 83. Kiongozi huyo wa kanisa katoliki amekuwa anasongwa na malalamiko kutoka duniani kote na kutakiwa kuyashughulikia huku mkazo ukiwa katika kuweka mambo bayana.

Asasi ya kutetea haki za wahanga, SNAP, imesema mageuzi hayo yanaashiria hatua muhimu inayoelekea upande sahihi. Hata hivyo asasi hiyo imesema mageuzi hayo bado hayajaanza kutekelezwa kwani bado ni maandishi tu, kinachotakiwa sasa ni hatua thabiti. Mnamo mwezi May kanisa katoliki lilitoa sheria nyingine kueleza wazi kwamba waliotendewa uhalifu wa kingono hawawezi kunyamazishwa na kwamba wanayo haki ya kujua matokeo ya kesi zao.

Vyanzo:/AP/RTRE