Papa Francis ayataka mataifa ya kigeni kuacha kuipora Kongo
1 Februari 2023Matamshi hayo ameyatoa siku ya Jumanne baada ya kuwasili kwenye mji mkuu wa Kongo, Kinshasa, katika ziara yake ya siku sita barani Afrika. Akizungumza na viongozi wa serikali, wanasiasa, wanadiplomasia, pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia na mashirika ya kimataifa, katika Ikulu ya Kongo, Papa Francis amesema ni jambo la kusikitisha kwamba bara la Afrika linaendelea kuvumilia aina mbalimbali za unyonyaji wa kisiasa ambao umetoa nafasi kwa kile alichokiita 'ukoloni wa kiuchumi' ambao ni sawa na utumwa.
Bara la Afrika halinufaiki na utajiri wake
Kiongozi huyo wa Kanisa katoliki duniani mwenye umri wa miaka 86, amesema Kongo hainufaiki na utajiri mkubwa wa rasilimali zake na madini yake kwa sababu ya sumu ya uchoyo, inayochochea mzozo nchini humo na kwamba mataifa tajiri hayawezi tena kufumbia macho hali mbaya ya mataifa mengi ya Afrika.
Ametaka wanaonufaika na rasilimali hizo kuacha kuikaba koo Kongo na Afrika kwa ujumla, kwani bara hilo sio mgodi wala eneo lenye ardhi ya kuporwa.
Kwa mujibu wa Papa, umefika wakati sasa wa kuondoa mirija ya unyonyaji Kongo na Afrika ili Waafrika wenyewe waweze kuwa wadau wa ustawi, maendeleo na mafao yao wenyewe na ulimwengu utambue kwamba kwa miaka mingi bara la Afrika limenyonywa, na hivyo tabia hiyo lazima sasa ifikie ukomo wake.
Aidha, Rais wa Kongo Felix Tshisekedi, pia ameishutumu jumuia ya kimataifa kwa kuisahau Kongo na kutochukua hatua kutokana na kukaa kimya kuhusu ukatili unaoendelea kwenye eneo la mashariki mwa nchi hiyo. ''Mbali na makundi yenye silaha, mataifa ya kigeni yenye uchu wa madini katika ardhi yetu, yanafanya ukatili mkubwa kwa msaada wa moja kwa moja wa jirani yetu Rwanda, hali inayolifanya suala la usalama kuwa changamoto kubwa kwa serikali,'' alifafanua Tshisekedi.
Kabla ya kutoa hotuba hiyo, Papa Francis alilakiwa na maelfu ya watu waliokuwa wamejipanga barabarani huku wakimshangilia. Jumatano asubuhi, Papa Francis ataongoza Ibada ya Misa Takatifu katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Ndolo, ambako zaidi ya waumini wapatao milioni mbili wanatarajiwa kuhudhuria, katika moja ya mikusanyiko mikubwa kabisa ya aina yake kuwahi kushuhudiwa nchini Kongo na moja ya Ibada kubwa zaidi ya Papa Francis kuwahi kutokea. Takribani nusu ya wananchi milioni 90 wa Kongo ni waumini wa madhehebu ya Kanisa Katoliki.
Papa kukutana na wahanga wa machafuko kutoka eneo la mashariki
Baba Mtakatifu alitarajiwa kuuzuru mji wa Goma ulioko mashariki mwa Kongo, lakini mazingira ya usalama katika jimbo la Kivu Kaskazini yamegubikwa na mapigano kati ya vikosi vya serikali na kundi la waasi wa M23, pamoja na mashambulizi ya wanamgambo wanaofungamana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.
Badala ya kuizuru Goma, Papa Francis atakutana na ujumbe wa watu kutoka eneo la mashariki ya Kongo waliosafiri kwenda Kinshasa kwa mkutano wa faragha na kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani utakaofanyika kwenye ubalozi wa Vatican baadae leo.
Papa Francis atakamilisha ziara yake ya Kongo siku ya Ijumaa, na kuelekea Juba, Sudan Kusini, nchi nyingine ya Afrika ambayo pia inakabiliwa na machafuko na umaskini. Kwenye nchi hizo, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani anapeleka ujumbe wa amani.
(AFP, AP, DPA, Reuters)