Poland na Ukraine zataka nyuklia ya Urusi iwekewe vikwazo
2 Machi 2023Nchi hizo zimeelezea pia hofu kwamba Urusi inaweza kuathiri usalama wa nishati na uchumi wa Ulaya ikiwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine yataendelea.
Hayo yameelezwa wakati wa kongamano la nishati katika mji mkuu wa Croatia, Zagreb, ambapo waziri wa mazingira wa Poland Anna Moskwa ametoa wito wa kusitisha uanachama wa Urusi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti nguvu za Atomiki, IAEA.
"Tunahitaji kusitisha ushirikiano wowote wa nyuklia na Urusi, tunahitaji kutokomeza sifa hii, kwa sababu hii ni moja ya changamoto tunayohitaji kukabiliana nayo kwa pamoja, na nadhani Ulaya itaweza kufanya hivyo. Lakini sio tu Ulaya, bali ulimwengu wote wa kidemokrasia. Kwa hivyo katika vikwazo vijavyo, kuwemo vya nyuklia," alisema Moskwa.
Waziri wa nishati wa Ukraine Germa Galushchenko, amesema wanapaswa kuiondoa Urusi katika sekta ya nyuklia na kwamba katika ulimwengu wa kistaarabu, Urusi haipaswi kuwa kama mshirika wa kibiashara.