Polisi yaanza kuwahamisha wakimbizi kisiwani Lesbos
17 Septemba 2020Polisi imesema operesheni hiyo ilioanza Alhamisi asubuhi inawajumuisha askari polisi wa kike 70 ambao wamekuwa wakiwafikia watafuta hifadhi ili kuwashawishi kwenda katika kambi ya muda ilioko eneo la Kara Tepe. Tangu kuanza kwa zoezi hilo, hakuna vurugu zozote ambazo zimeripotiwa.
"Hii ni oparesheni ya kulinda afya ya umma na ambayo pia ni ya kiutu” polisi imesema katika taarifa yake.
Mkuu wa shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika kisiwa hicho Astrid Castelein amesema amefurahiswa na hatua hiyo.
"Ili mradi zoezi hilo linafanyika kwa amani bila vurugu, tunaamini kwamba ni hatua nzuri ukizingatia kwamba katika mitaa wanakolala wakimbizi kuna hatari ya usalama wao pamoja na hatari ya afya kwa umma” amesema mkuu huyo.
Inaarifiwa kuwa hadi kufikia Alkhamis asubuhi watu wapatao 459 tayari wamehamishwa hadi eneo la Kara Tepe kati yao, 250 wakiwa tayari wameingia katika kambi baada ya kupimwa virusi vya Corona. Wengine walikuwa bado wanasubiri kuingia na wakimbizi wengine pia wakitarajiwa kuwasili.
Mnamo wiki iliyopita kambi ya wakimbizi ya Moria iliteketea moto. Lakini mamlaka za Ugiriki inasema moto huo uliwashswa maksudi na kikundi kidogo cha wakimbizi katika kambi hiyo ambao walighadhabishwa na vizuizi vya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Corona. Vizuizi hivyo viliwekwa baada ya kuzuka visa vya COVID-19 katika kambi hiyo.
Moto huo, umewaacha zaidi ya wakimbizi 1,200 wakihitaji makazi ya dharura na wengi wao wamekuwa wakilala nje katika barabara ya kutoka kambi hiyo kuelekea mji mkuu wa kisiwa Lesbos, Mytilene.
Kulingana na shirika la kuwadumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa hadi kufikia Juma tano usiku kambi mpya ilikuwa na uwezo wa kuwahifadhi watu 8,000 lakini ni watu 1,100 pekee hasa waliomo hatari zaidi ndio waliokuwa wameingia katika kambi hiyo. Kila wanaoingia kambi hiyo hupimwa virusi vya Corona na kisha kupewa hema.
Wakati huo huo, shirika la madaktari wasio na mipaka limesema polisi wa Ugiriki ilikuwa inawazuwia wafanyakazi wake kuifikia zahanati yake katika kisiwa hicho.
"Sisi ndio shirika pekee la kimatibabu katika kisiwa hicho lakini tunaendelea kuzuiliwa, watu wengi wanahitaji misaada ya kimatibabu lakini hatuwezi kuwafikia, kwanini polisi inatuzuwia? Shirika hilo limeandika kwenye mtandao wake wa twitter.
Raia sita wa Afghanistan wakiwemo watoto wawili wametiliwa nguvuni wakishukiwa kuwa ndio waliowasha moto huo uliookea wiki iliyopita.
Moto huo ulizuka baada ya kutolewa kwa amri ya kujitenga katika wakati ambapo kambi hiyo tayari ilikuwa chini ya vizuizi baada ya watu 35 kukutwa na virusi vya Corona.
Kambi ya Moria ilikuwa na uwezo wa kuwahifadhi watu 2,700 lakini zaidi ya watu 12,500 ndio waliokuwa wakiishi ndani na je yake wakati ilipochomeka. Wakosoaji wamesema kambi ya Moria ambayo ilikuwa imejaza wakimbizi kupita kiasi ni ishara inayo onyesha kufeli kwa sera za Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi.
Kwa muda murefu Ugiriki imekuwa ikitaka kuongezeka kwa mshikamano kutoka kwa mataifa mengine ya Umoja huo kuhusu suala la wakimbizi.
Ugiriki inasema haipaswi kuachwa pekee yake kulishughulikia suala la uhamiaji kwa sababu tu ya eneo lake la kijiografia yaani katika mpaka wa kusini mashariki wa Umoja huo, ambako wakimbizi wengi hupitia.
Chanzo: AP