1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki: Ulaya ionyeshe mshikamano wa vitendo

15 Septemba 2020

Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis amesema bara la Ulaya linapaswa kuionyesha Ugiriki mshikamano kwa vitendo katika mzozo wa wahamiaji, baada ya moto kuiunguza kambi ya wakimbizi ya Moria, wiki moja iliyopita.

https://p.dw.com/p/3iVfE
Griechenland Athen Parlament | Kyriakos Mitsotakis, Premierminister
Picha: Reuters/C. Baltas

Akizungumza baada ya kukutana na Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, Mitsotakis amesema ni muda kwa Ulaya kuiunga mkono kwa vitendo linapokuja suala la wakimbizi na sio maneno. Amesema kuwa kambi ya wakimbizi ya Moria iliyoko kwenye kisiwa cha Lesbos imeharibika kabisa na kwamba kambi mpya itajengwa, kwa msaada na ushiriki wa Umoja wa Ulaya.

''Tunapaswa tuuangalie ukweli moja kwa moja. Ni muda kwa Ulaya kutuunga mkono kwa vitendo ili tuweze kusonga mbele. Tuwe na mshikamani unaoonekana. Sera mpya ya wahamiaji, utambulisho, utoaji hifadhi na hatua ya wakimbizi kuhamishwa inahitajika. Tunasubiri mapendekezo ya Halmashauri kwa hamu kubwa,'' alisisitiza Mitsotakis

Mitsotakis amesema hadi sasa wahamiaji wapatao 800 walioachwa bila makaazi wamehamishiwa kwenye eneo ambalo limejengwa na jeshi la Ugiriki na kwenye kituo hicho kuna mahema tu.

Kwa upande wake Michel amesema nchi zote wanachama za Umoja wa Ulaya zinapaswa kugawana mzigo wa kupambana na changamoto za uhamiaji. Amebainisha kuwa suala la uhamiaji sio tu changamoto kwa nchi kadhaa wanachama zilizoko kwenye mstari wa mbele, lakini pia kwa Umoja wa Ulaya kwa ujumla.

Angela Merkel CDU und Horst Seehofer CSU
Horst Seehofer na Kansela Angela MerkelPicha: Getty Images/S. Gallup

Kwa upande wake Ujerumani imekubali kuwachukuwa wahamiaji wengine 1,500 ambao kwa sasa wamekwama nchini Ugiriki. Shirika la habari la Ujerumani DPA, limesema kwamba Kansela Angela Merkel na Waziri wa Mambo ya Ndani, Horst Seehofer wamekubaliana kuwachukuwa wakimbizi hao walioko kwenye kisiwa cha Ugiriki, baada ya moto kusababisha maelfu kukosa mahali pa kuishi.

Merkel na Seehofer wameufikia uamuazi huo baada ya shutuma kwamba serikali ya Ujerumani haijafanya vya kutosha kuwasaidia wakimbizi hao. Hatua hiyo inaziangazia zaidi familia zenye watoto. Jumla ya watu 12,000 wameachwa bila makaazi baada ya moto huo kuzuka. Mara tu baada ya mkasa huo ambao uliiteketeza kabisa kambi hiyo, Ujerumani ilikuwa imetangaza kwamba iko tayari kuwachukuwa watoto 150 wasiokuwa na walezi miongoni mwa wakimbizi hao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema kuna haja ya kuchukua hatua za haraka kuwanusuru wakimbizi hao ambao wameachwa bila ya makaazi, mahali safi au bila ya kupata chakula na maji baada ya mkasa huo kutokea. Wengi wa wakimbizi hao ni kutoka Afghanistan, Afrika na Syria.

(AP, AFP, DPA, Reuters)