Putin adai ushindi katika kulinda Kazakhstan dhidi ya uasi
10 Januari 2022Putin ameuambia Mkutano wa kilele uliofanyika kwa njia ya video ukiwahusisha wakuu wa nchi za muungano wa kijeshi wa mataifa yaliokuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti, CSTO, kwamba chombo hicho kimefanikiwa kuzuwia kile alichokiita kudhoofishwa kwa misingi ya taifa, kuvurugwa kabisaa kwa ahali nchini Kazakhstan na umezuwia magaidi, wahalifu na waporaji na wahalifu wengine.
"Bila shaka, tunaelewa kwamba matukio nchini Kazakhstan siyo jaribio la kwanza na la mwisho la uingiliaji wa nje katika masuala ya ndani ya mataifa yetu. Hatua ambazo CSTO ilizichukuwa zimeweka wazi kwamba hatutomruhusu yeyote kuvurga hali nyumbani kwetu na kutekeleza matukio ya kile kinachoitwa mapinduzi ya rangi," alisema Putin.
Mamlaka nchini Kazakhstan zimesema siku ya Jumatatu kwamba karibu watu 8,000 wamekamatwa na polisi wakati wa maandamano yaliogeuka kuwa machafuko mabaya zaidi kushuhudiwa na taifa hilo la zamani la Kisovieti, tangu kujipatia uhuru wake miaka 30 iliyopita.
Soma pia: Kazakhstan: Zaidi ya 160 wauawa, 8,000 wakamatwa
Rais Kassym-Jomart Tokayev ameyaelezea matukio ya wiki iliyopita kama uvamizi wa kigaidi dhidi ya taifa lake, na kutupilia mbali ripoti kwamba mamlaka zilipambana na waandamanaji wa amani, akizitaja kuwa upotoshaji. Wizara ya afya ya nchi hiyo ilisema Jumapili kwamba watu 164 waliuawa katika machafuko hayo, wakiwemo watoto watatu.
Serikali ya Kazakhstan ilitangaza hali ya hatari kuhusiana na machafuko hayo, na Tokayev aliomba msaada kutoka CSTO. Jumuiya hiyo iliidhinisha kutumwa kwa wanajeshi 2,500 wengi wao kutoka Urusi, kwenda nchini Kazakhstan.
Magharibi yanyooshewa kidole
Urusi na Kazakhstan zote zimeyaonyesha machafuko hayo kama uasi ulioungwa mkono na magharibi, ingawa hawajasema nani wanamlaumu kwa kuyapanga.
Urusi kwa muda mrefu imezilaumu nchini za Magharibi kwa kuchochea kile kinachoitwa mapinduzi ya rangi, ambayo yamepindua serikali katika mataifa kama vile Georgia, Ukraine, Kyrgyzstan na Armenia -- na kuimarisha jukumu lake katika kusaidia kuyakandamiza.
Soma pia: Tokayaev apuuza mazungumzo na waandamanaji Kazakhstan
Urusi ilimuunga mkono kiongozi wa Belarus katika kusambaratisha maandamano ya mwaka 2020. Lukashenko ambaye amehudhuria pia mkutano wa kilele wa CSTO, na ametoa wito wa kuimarishwa kwa muungano huo na kuchukua hatua bila kuyaangalia mataifa ya Magharibi.
Putin amesema majeshi ya kulinda amani ya CSTO yamewekwa Kazakhstan kwa muda tu na kwamba yataondoka nchini humo mara baada ya kumaliza kazi yake.
Chanzo: Mashirika