1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Putin afanya mazungumzo ya nadra na Waziri Mkuu wa Slovakia

23 Desemba 2024

Rais wa Urusi amekuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico katika ziara ya nadra ya kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya katika ikulu ya Kremlin tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari mwaka 2022.

https://p.dw.com/p/4oUVT
Urusi | 2024 | Slovakia | Fico | Putin
Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico akikutana na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Artyom Geodakyan/TASS/IMAGO

Fico amekuwa kiongozi wa tatu kutoka Umoja wa Ulaya kukutana na rais Putin tangu uvamizi kamili wa Ukraine miaka mitatu iliyopita.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov ameliambia shirika la habari la Urusi RIA kuwa Waziri Mkuu huyo wa Slovakia aliwasili Urusi kwa ziara ya kikazi na alikutana na Putin jana jioni.

Kulingana na Peskov, mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yalijikita juu ya masuala ya "hali ilivyo kimataifa” na usambazaji wa gesi asilia ya Urusi.

Waziri Mkuu huyo wa Slovakia – mkosoaji mkubwa wa uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya kwa serikali ya Kyiv – amesema walijadiliana kuhusu usambazaji wa gesi ya Urusi kwenda Slovakia, ambayo nchi yake inaitegemea.

Soma pia: Maoni: Putin amepoteza vita vya gesi na Ujerumani 

Fico aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook baada ya kukutana na Putin kwamba, aliwaeleza viongozi wa Umoja wa Ulaya kuhusu ziara yake mjini Moscow.

Gesi asilia ya Urusi bado inasafarishwa kuelekea baadhi ya nchi za Ulaya, ikiwemo Slovakia, kupitia Ukraine kwa mujibu wa makubaliano ya miaka mitano yaliyotiwa saini kabla ya vita na ambayo yanatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Mkataba wa kusafirisha gesi kuisha mwishoni mwa mwaka huu

Urusi | Gazprom
Mfanyakazi wa kampuni ya gesi ya Urusi GazpromPicha: Maxim Shipenkov/epa/dpa/picture-alliance

Mkataba na kampuni kubwa ya gesi ya Urusi ya Gazprom ya kusafirisha nishati hiyo kupitia Ukraine hadi Slovakia unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Fico amesema mkutano huo wa mjini Moscow ni jibu kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alipowaambia viongozi wa Umoja wa Ulaya kwamba Ukraine inapinga gesi ya Urusi kupitishwa katika eneo lake.

Waziri Mkuu huyo wa Slovakia, ambaye alinusurika kupigwa risasi mapema mwaka huu, ameeleza kuwa alifanya mazungumzo marefu na Putin na kwamba wawili hao walibadilishana mawazo kuhusu hali ya kijeshi ilivyo nchini Ukraine.

Soma pia: Urusi yakamilisha ujenzi wa bomba la gesi la Nord Stream 2 

Viongozi hao wawili walijadili pia juu ya "uwezekano wa mapema na kwa njia ya amani ya kuvimaliza vita hivyo” na uhusiano kati ya Urusi na Slovakia, Fico aliandika kwenye mtandao wake wa Facebook.

Slovakia na Hungary, ambazo zote zinategemea gesi ya Urusi, zimeibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa usambazaji wa gesi hiyo kukatizwa.

Mnamo mwaka 2023, wakati Fico alipokuwa Waziri mkuu tena, alisitisha msaada wa kijeshi wa Slovakia kwa Ukraine.

Hata hivyo wakati huo alisisitiza kuwa anataka kuwa Jirani mwema kwa Ukraine. Mkutano wa Fico na Putin unatokea wakati viongozi wa Italia, Uswidi, Ugiriki na Finland walipokutana jana kwa mkutano wa kilele wa usalama.