Putin: Urusi iko tayari kwa vita vya nyuklia
13 Machi 2024Kauli ya Vladimir Putin ni kama onyo la wazi kwa nchi za Magharibi kabla ya uchaguzi mkuu wa rais wiki hii nchini Urusi ambapo Putin ana uhakika wa kujishindia muhula mwingine wa miaka sita madarakani.
Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha serikali ya Urusi yaliyopeperushwa mapema leo, Putin alimuelezea Rais Joe Biden wa Marekani kama mwanasiasa mkongwe anaelewa kikamilifu hatari zinazoweza kutokea ikiwa mzozo utatanuka lakini akasema kuwa hafikirii kuwa ulimwengu unaelekea kwenye vita vya nyuklia.
Wakati huo huo, rais Putin amesisitiza kuwa vikosi vyenye dhamana ya silaha za nyuklia vya Urusi vimejitayarisha kikamilifu huku akisema kuwa mifumo ya silaha za nyuklia ya Urusi iwe ya angani, majini na ardhini ni bora zaidi:
" Kwa mtazamo wa kijeshi na kiufundi, bila shaka, tuko tayari kwa vita vya nyuklia. Wanajeshi wa Urusi daima wako katika hali ya utayari wa kupambana. Hili ndilo jambo la kwanza. Pili, kwa ujumla, mifumo yetu ya nyuklia ni ya kisasa zaidi kuliko mingine yoyote. Ni sisi tu na Marekani ambao tuna mifumo kama hii. Lakini mifumo yetu ni ya kisasa zaidi."
Kiongozi huyo wa Urusi amekuwa mara kwa mara akielezea juu ya utayari wake wa kutumia silaha za nyuklia tangu alipoivamia Ukraine mwezi Februari mwaka 2022.
Soma pia: Putin asifu mafanikio Ukraine, atishia vita vya nyuklia
Aidha, rais huyo wa Urusi ameendelea kusema ikiwa washirika wa Ukraine watatuma wanajeshi kuisaidia nchi hiyo iliyokumbwa na vita, hilo halitobadili matokeo katika uwanja wa vita kama ilivyokuwa kwa hatua yao ya kuipatia Ukraine silaha.
Mapambano makali yaendelea
Ukraine imeendeleza mashambulizi yake ndani ya ardhi ya Urusi na kuilenga miundombinu ya nishati hasa viwanda vya uchimbaji na usafishaji mafuta ghafi.
Siku ya Jumatano, droni ya Ukraine imelishambulia jengo kunakopatikana idara ya usalama ya Urusi FSB katika mji wa mpakani wa Belgorod.
Soma pia: Urusi: Sera za Marekani na washirika wake zatishia matumizi ya silaha za nyuklia
Rais Vladimir Putin amesema Ukraine inaongeza mashambulizi yake katika ardhi ya Urusi ili kujaribu kuvuruga uchaguzi ujao wa rais unaotarajiwa kufanyika tarehe 13 hadi 17 mwezi huu wa Machi.
Hata hivyo, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imefanikiwa kudungua usiku wa kuamkia leo droni 58 za Ukraine zilizokuwa ziliyalenga maeneo ya Belgorod, Bryansk, mikoa ya Voronezh, Kursk, Ryazan, na Leningrad. Pia, watu kadhaa wameripotiwa kufariki usiku wa kuamkia leo nchini Ukraine kufuatia mashambulizi mapya ya Urusi.
(Vyanzo: Mashirika)