Mazungumzo ya kuongeza muda wa kusitisha vita Gaza yaendelea
30 Novemba 2023Mkuu wa idara ya habari ya Misri Diaa Rashwan amesema kurefushwa kwa muda wa usitishaji wa mapigano kwa siku mbili zaidi ni juhudi zinazofanywa ili kuwawezesha wafungwa wengi zaidi na mateka kuachiliwa huru na kuingiza misaada mingi zaidi ya kiutu katika Ukanda wa Gaza.
Soma zaidi: UN: Kuundwe mataifa mawili katika mzozo wa Israel-Hamas
Wakati mazungumzo hayo ya kuongeza muda zaidi wa kusimamisha vita yakiendelea, shirika la hilali nyekundu la Palestina limesema kuwa malori 1,132 yaliyobeba misaada ya kiutu kwa ajili ya Ukanda wa Gaza yameingia katika ukanda huo kupitia mpaka wa Rafa tangu mapigano yaliposimamishwa kwa muda.
Blinken apongeza kuongeza muda wa usitishwaji vita
Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema kuwa makubaliano ya usitishwaji vita kati ya Israel na kundi la Hamas yanaonesha matokeo na yanapaswa kuendelea.
Blinken ameyasema hayo mjini Tel Aviv wakati alipokutana na rais wa Rais Isaac Herzog.
Blinken alikutana pia na kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliyesisitiza kuwa wataendeleza vita hadi malengo ya kuachiliwa mateka, kuliangamiza kundi la Hamas na kuhakikisha kwamba Gaza haitakabiliwa na kitisho kama hicho yatakapotimia.
Katika ziara yake ya tatu tangu mzozo kati ya Israel na hamas ulipoanza, Blinken anatarajiwa pia kukutana na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.
Kwingineko Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock amepongeza hatua ya kurefushwa kwa muda wa usitishaji wa vita katika ukanda wa Gaza. Baerbock amesema amani kwa Waisrael na Wapalestina inategemea kupatikana kwa suluhisho la pamoja la kuhakikisha kunakuwa na usalama katika pande hizo mbili.