1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia 22 wauawa kinyama DRC

26 Desemba 2016

Takriban watu 22 wameuwawa katika jimbo la Kaskazini la Kivu katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Waasi wa Uganda wamelaumiwa kwa kufanya mauaji hayo ya kinyama.

https://p.dw.com/p/2UsU1
Symbolbild Opfer der ADF
Picha: Getty Images/AFP/K. Mailro

Kwa mujibu wa afisa wa serikali Amisi Kalonda,  mji wa Beni umekabiliwa na mashambulio ya mara kwa mara ambapo hadi sasa zaidi ya watu mia saba wameuwawa.  Wapiganaji wa kundi la waasi la Allied Democratic Forces ADF, ambalo ni kundi la Kiislamu lenye itikadi kali kutoka nchini Uganda wanaendeleza vitendo vya ukatili dhidi ya raia kwa karibu miongo miwili sasa.  Kundi hilo liliuvamia mji huo wa Eringeti na maeneo yanayouzunguuka siku ya Jumamosi. watu 10 waliuwawa katika mji huo wa Eringeti huku maiti za watu wengine 12 zilipatikana katika maeneo ya karibu na mji huo.

Kundi hilo hutumia mtindo mmoja katika mauaji ya raia, linawauwa watu kwa kuwachoma visu au kwa kuwakata mapanga.  Kwa miaka miwili sasa eneo la Beni na miji inayouzunguuka mji huo imekumbwa na mauaji ya watu wengi ambapo mamia ya raia wameuwawa kinyama wengi wao kwa kunyongwa.  Maafisa wa serikali ya Kongo wanawalaumu wapiganaji wa kundi la ADF lakini wataalamu kadhaa wametoa taarifa kuwa hata makundi mengine ikiwa ni pamoja na jeshi la serikali ya Kongo yanahusika na baadhi ya mauaji hayo. 

Kongo Afrika Massaker Mann sitzt vor einer ausgebrannten Hütte
Wakaazi wa Beni katika maandamano kupinga mauaji dhidi ya raia wenzao Agosti 15, 2016. Kundi la ADF linalaumiwa kufanya mauaji hayo.Picha: Getty Images/K.Maliro

Msemaji wa jeshi la Kongo Mak Hazukay amethibitisha mashambulio hayo ya Jumamosi na wakati huo huo amearifu kwamba jeshi limewauwa wapiganaji wanne wa kundi la ADF lakini amekiri kwamba idadi ya raia waliopoteza maisha ni kubwa. Msemaji huyo wa jeshi amesema kwamba jeshi lilihusika katika operesheni kwenye eneo la Beni ingawa hakutoa maelezo zaidi.

Mauaji ya kinyama katika mji wa Beni yalianza mnamo mwaka 2014 na mara moja serikali ya Kongo pamoja na  kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani MONUSCO walielekeza lawama kwa kundi la waasi la ADF lakini miaka miwili baadae serikali ya Kongo na Umoja wa Maataifa wameshindwa kabisa kuwalinda raia katika eneo hilo.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE

Mhariri:Iddi Ssessanga