Raia wa Iran waendelea kuandamana licha ya onyo la Mahakama
26 Septemba 2022Takriban watu 41 wamekufa tangu kuanza kwa maandamano hayo, wengi wao wakiwa waandamanaji lakini wakiwemo pia maafisa wa usalama wa Iran. Hii ni kwa mujibu wa idadi rasmi iliyotolewa, ingawa vyanzo vingine vinasema idadi halisi ni kubwa zaidi.
Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Iran (IHR) lenye makao yake makuu mjini Oslo nchini Norway, limesema jana jioni kuwa idadi ya waliofariki ni angalau 57, lakini ikabaini kuwa kukatika kwa mtandao wa intaneti kunafanya iwe vigumu kuthibitisha vifo wakati maandamano hayo yanayoongozwa na wanawake yakiwa yameenea katika miji kadhaa.
Soma zaidi: Watu 31 wauawa kwenye maandamano nchini Iran
Akirejelea onyo lililotolewa awali na Rais wa Iran Ebrahim Raisi, mkuu wa mahakama Gholamhossein Mohseni Ejei alisisitiza haja ya " kuchukuliwa hatua madhubuti na bila huruma" dhidi ya waanzilishi wa "machafuko hayo".
Mamia ya waandamanaji, wanaharakati wa mageuzi na waandishi wa habari wamekamatwa huku kushuhudiwa maandamano kila usiku tangu yalipozuka kwa mara ya kwanza Septemba 16 baada ya kifo cha Mahsa Amini aliyekuwa na umri wa miaka 22.
Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti leo kuwa mamlaka katika mkoa wa kaskazini mwa Iran wamewakamata watu 450.
Wanawake waungwa mkono duniani
Maandamano kama hayo ya kuwaunga mkono wanawake wa Iran yameripotiwa sehemu mbalimbali duniani.
Jana, Polisi wa Ufaransa walikabiliana na waandamanaji waliokadiriwa kufikia idadi ya 4000 waliokuwa wakijaribu kufika katika balozi za Iran mjini Paris. Polisi wa Ufaransa walitumia gesi ya kutoa machozi ili kuwazuia waandamanaji hao.
Hali sawa na hiyo iliripotiwa pia mjini London, ambapo polisi wa Uingereza walisema wamewakamata watu 12 huku maafisa watano "wakijeruhiwa vibaya" wakati waandamanaji walipojaribu kuvunja vizuizi vinavyolinda ubalozi wa Iran nchini humo.
Soma zaidi: Raisi aonya waandamanaji nchini Iran
Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema Marekani inajaribu kukiuka uhuru wa nchi hiyo kwa kuwaunga mkono waandamanaji na kuwa kufanya hivyo kunadhohofisha uthabiti na usalama, na kusisitiza kuwa hilo halitochwa bila majibu.
Maandamano makubwa zaidi
Maandamano haya ni makubwa zaidi kuwahi kutokea tangu yale ya mwaka 2019 yaliyokuwa yakipinga kupanda kwa bei ya mafuta na ambapo watu karibu 1500 waliuawa kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Maandamano ya sasa yamelaaniwa kimataifa lakini mamlaka nchini Iran inawalaumu wapinzani wa Kikurdi wenye silaha kuhusika katika machafuko yanayoendelea nchini humo, hasa katika maeneo ya kaskazini-magharibi ambapo karibu Wakurdi wa Iran hadi milioni 10 wanaishi maeneo hayo.
(AFPE, RTRE)