Rais Buhari akabiliwa na shinikizo la ukosefu wa usalama
3 Mei 2021Mashambulizi ya umwagaji damu na utekaji nyara vilishuhudiwa zaidi kwa karibu kila siku ya mwezi Aprili katika taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika la Nigeria. Wiki iliyopita pekee zaidi ya watu 240 wanakadiriwa kuwa waliuwawa na zaidi ya 48 walitekwa nyara kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo.
Kati ya waliouwawa ni pamoja na wafugaji 19 waliopigwa risasi kusini mashariki mwa jimbo la Anambra. Wanafunzi watano wa eneo la kaskazini magharibi walipigwa risasi baada ya kutekwa nyara na watu wenye silaha wakiwa chuoni, wanajeshi 32 waliuawa wakati wa shambulio la kushtukiza katika mkoa wa ziwa Chad, na wezi wa mifugo wakawauwa polisi 8 kaskazini magharibi mwa jimbo la Kebbi
Maseneta, na magavana wa majimbo na hata mshidi wa tuzo ya amani ya nobeli Wole Soyinka wametoa wito kwa Rais Buhari afanye juhudi zaidi ili kukabiliana na machafuko. Bunge nalo hivi karibuni lilimtaka atangaze hali ya hatari nchi nzima. Sauti nyingi zaidi za ukosoaji zimekuwa zikiuliza ni kwanini amiri jeshi huyo mkuu anaonekana lakini katika suala la usalama ni kama vile hayupo.Wanafunzi 279 waliotekwa nyara Nigeria waachiwa huru
Utekaji Nigeriwafikia kiwango cha mzozo
Wanafunzi watekwa tena Nigeria
Mmoja wa maseneta kutoka chama tawala cha Rais Buhari cha APC Smart Adeyemi anasema mgogoro wa sasa nchini humo ndio mbaya zaidi unaolikabili taifa hilo kwa sasa. Katika mkutano wa hivi karibuni kwa njia ya video kati yake na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken, Rais huyo wa Nigeria alisema jeshi lina nia thabiti ya kukabiliana na ukosefu wa usalama huku akitaka ushirikiano zaidi na washirika wa mataifa ya kigeni. Lakini raia wengi wa Nigeria wanalalamikia kile wanachokiita ombwe la uongozi.
Mshindi wa tuzo ya Nobeli Wole Soyinka katika kauli yake inayotafsiriwa kama fumbo kwa Rais Buhari anasema, wale wanaothibitika kuwa ni dhaifu wanapaswa kuweka pembeni majivuno yao, watafute usaidizi na waache kuchezea maisha ya raia.
Mnamo mwaka 2015, Buhari alipoingia madarakani, wengi walimuona kama mtu sahihi katika nafasi ya kuliongoza taifa hilo, ni kamanda wa jeshi na alikuwa na sifa sahihi katika masuala ya usalama. Alitangaza mapema kwamba uasi wa makundi ya kiislamu yenye siasa kali hayapo tena. Lakini hata wakati wa mhula wake wa kwanza tu, alikosolewa na wapinzani wake kwa mtindo wake wa kutokuchukua hatua na kujihami katika kukabiliana na changamoto za kiusalama.
Ndani ya miaka sita tangu alipoingia madarakani, changamoto za usalama zimezidi kushamiri Nigeria. Wachambuzi wanasema, uchumi wa nuliodhoofishwa na kushuka kwa bei za mafuta na janga la COVID 19 pamoja na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira vinazidi kuleta migogoro kwenye baina ya jamii hasimu. Matokeo yake, magenge ya uhalifu yanaongezeka.
Nigeria imekuwa ikipambana kukomesha makundi ya wanamgambo wenye siasa kali katika eneo la kaskazini mashariki kwa zaidi ya muongo mmoja sasa. Kutokana na Mzozo nchini humo, watu 36,000 wameuwawa na zaidi ya wengine milioni mbili hawana makazi na wamelazimika kutawanyika katika mataifa mengine kama vile Chad, Niger na Cameroon.