Biden alalamikia vizingiti vinaavyowekwa na utawala wa Trump
29 Desemba 2020Rais mteule wa Marekani Joe Biden amelalamika juu ya vizingiti vinavyowekwa na utawala wa Trump katika kipindi cha mpito. Biden amesema mashirika ya usalama yamehujumiwa chini ya utawala wa Trump na ameeleza kuwa ni kitendo cha kutowajibika kuzuia ripoti kwa utawala ujao. Ameeleza kuwa timu yake inakabiliwa na vizingiti kwenye serikali ya Trump, kuanzia kwenye wizara ya ulinzi hadi kwenye idara za usimamizi na bajeti.
Soma Zaidi: Joe Biden athibitishwa rasmi kuwa rais ajae wa Marekani
Rais mteule Biden alisema hayo baada ya kukutana na timu yake itakayoshughulikia masuala ya nchi za nje, usalama wa taifa, ulinzi na washauri wake, wakiwemo mawaziri wake wateule wa mambo ya nje, ulinzi, mambo ya ndani pamoja na mshauri wa usalama wa nchi ajae.
Amesema kwa sasa hawapati ripoti zote zinazohitajika juu ya maeneo muhimu ya usalama kutoka kwa utawala wa Trump unaokaribia kuondoka madarakani. Amesisitiza kwamba kikosi chake kinahitaji ripoti zote juu ya mchakato wa bajeti ya wizara ya ulinzi
Mpaka sasa rais Trump bado amekataa kukubali kuwa alishindwa kwenye uchaguzi kwa zaidi ya kura milioni 7, na utawala wake haukuidhinisha mapema ushirikiano rasmi na timu ya mpito ya Biden hadi Novemba 23, wiki baada ya uchaguzi.
Biden amesisitiza kuwa changamoto kuu itakayowakabili yeye na makamu wake wa rais Kamala Harris ni kuzijenga upya idara za mambo ya nje na ile ya usalama wa taifa mara watakapoanza kazi mnamo Januari 20 mwakani.
Vyanzo:/AP/https://p.dw.com/p/3nIk3