Jair Bolsonaro arejea Brazil kuuongoza upinzani
30 Machi 2023Bolsonaro alikaribishwa na mamnia ya wafuasi wake kwenye uwanja wa ndege wa Brasilia siku ya Alhamisi huku kukiwa na ulinzi mkali. Kwa mujibu wa maafisa wa chama chake cha Partido Liberal (PL) wamesema Rais huyo wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro, ambaye hakuwahi kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa mwaka jana ataongoza upande wa upinzani dhidi ya Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva.
Bolsonaro aliondoka Brazil muda mfupi kabla ya muhula wake madarakani kukamilika. Hatua hiyo ilikiuka desturi na kuonesha kuwa kwa makusudi alikataa kukabidhi uongozi kwa mrithi wake, Luiz Inacio Lula da Silva, ambaye alishinda uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2022.
Akiwa nchini Marekani, Bolsonaro mara nyingi alijiepusha kutoa matamko hadharani ingawa alitoa hotuba kadhaa kwa wataalamu wa Brazil na wahafidhina ikiwa ni pamoja na katika Mkutano wa Kihafidhina wa katika jiji la Maryland.
Hata hivyo makusudio ya Bolsonaro ya kurudisha umaarufu wake wa kisiasa yanaweza kukwama kutokana na kukabiliwa na mfululizo wa uchunguzi dhidi yake, ikiwa ni pamoja na kuchunguzwa iwapo alichochea uasi wa Januari 8.
Soma:Polisi wachunguza vito vya thamani vya Bolsonaro vilivyoingizwa Brazil
Hivi majuzi gazeti la Estado de S.Paulo lilifichua kuhusu masanduku matatu yaliyojaa vito vya gharama kubwa yanayodaiwa kuletwa kwa Bolsonaro kutoka Saudi Arabia hali ambayo inamuweka hatarini rais huyo wa zamani kufuatwa na mkondo wa sheria.
Steve Bannon, mshirika wa muda mrefu warais wa zamani wa Marekani Donakd Trump ameliambia gazeti la Brazil, Folha de S.Paulo kwamba Bolsonaro kamwe hakupaswa kuondoka nchini, na kwamba hakuna umuhimu wa kuchumchunguza kiongozi huyo.
Mbali na uchunguzi kuhusu vito vya almasi, Bolsonaro anakabiliwa na takriban tuhuma kumi na mbili zilizowasilishwa na mahakama zinazohusiana na matendo yake wakati wa kampeni za uchaguzi za mwaka jana hasa kuhusiana na madai yake ambayo hajayathibitishwa kuwa mfumo wa kielektroniki wa kupiga kura ulikuwa wa udanganyifu.
Ikiwa Bolsonaro atapatikana na hatia katika yoyote kati ya kesi hizo anaweza kupoteza haki zake za kisiasa na kuzuiwa kugombea urais katika uchaguzi ujao.
Vyanzo:AFP/AP/RTRE