1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto asema hakutakuwa na ubaguzi katika utawala wake

3 Oktoba 2022

Rais wa Kenya William Ruto ameahidi kuwa serikali yake kamwe haitombagua wala kuwaacha nje ya mipango ya maendeleo ya kitaifa raia wa maeneo fulani nchini humo licha ya tofauti za kisiasa zilizopo

https://p.dw.com/p/4Hgef
Kenia wartet mit Spannung auf das Urteil des Obersten Gerichtshofs zu den Wahlen | William Ruto
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Akizungumza katika ziara yake ya kwanza eneo la Nyanza - ngome ya kinara wa muungano wa kisiasa wa Azimio Raila Odinga, jimboni Homabay, Ruto amesisitiza kuwa, kama rais wa taifa la Kenya ana wajibu wa kuwashugulikia Wakenya wote bila kikwazo wala ubaguzi wowote.

Kuwekea msisitizo wa ahadi yake, Ruto amewaahidi wakaazi wa eneo hilo kwamba, msururu wa miradi na mipango ikiwemo ya Barabara, makaazi ya bei nafuu, kilimo, kuekeza katika taasisi za elimu ya juu, maji miongoni mwa miradi mingine.

Kadhalika, Rais Ruto alitumia fursa hiyo kueleza kuwa, serikali yake inawaheshimu na kwamba itawaangalia vizuri rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kinara wa muungano wa Azimio Raila Odinga ikiwemo kuwaandalia mazingira tulivu ya kushirikishwa katika majukumu mengine ya taifa. 

soma zaidi:William Ruto aapishwa kuwa Rais wa Kenya

Kwenye ziara hiyo, Ruto aliandamana na viongozi mbali mbali wa eneo la Nyanza akiwemo David Ochieng mbunge wa Ugenya miongoni mwa wengine ambao wamesema watashirikiana na rais kuhusu maswala ikiwemo uvuvi, kilimo cha pamba, nafasi za uimarishaji miongoni mwa wanawake na vijana. 

Rais Ruto ameahidi pia kushirikiana na viongozi wa kidini eneo hilo.

Mwandishi: Musa Naviye