1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Rais Xi achaguliwa tena kwa muhula wa tatu kuongoza China

10 Machi 2023

Rais wa China amekabidhiwa leo muhula wa tatu kuiongoza China, hatua inayomfanya kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi katika vizazi vingi nchini humo.

https://p.dw.com/p/4OUXP
China | 14. Nationaler Volkskongress |  Xi Jinping
Picha: Noel Celis/AFP/Getty Images

Kuthibitishwa kwake na bunge la taifa kumejiri baada ya Rais Xi kukabidhiwa hatamu nyingine ya kukiongoza chama chake cha Kikomunisti mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita kwa miaka mingine mitano.

Kando na wajumbe kumkabidhi Rais Xi Jinping mwenye umri wa miaka 69, muhula wa tatu kuwa rais, pia walimchagua kwa kauli moja na kumteua tena kuwa mkuu wa tume kuu ya kijeshi nchini humo.

Tangazo la matokeo ya kura kwenye Ukumbi mkuu wa Beijing, lilionesha kwamba wajumbe wote 2, 952 walipiga kura kwa kauli moja kumpa Xi muhula mwingine madarakani.

Wabunge wote wamemchagua Rais Xi Jinping kuwa rais na mkuu wa Tume kuu ya kijeshi wa China.
Wabunge wote wamemchagua Rais Xi Jinping kuwa rais na mkuu wa Tume kuu ya kijeshi wa China.Picha: Mark Schiefelbein/AP/picture alliance

Kwenye kiapo chake, Xi aliahidi kujenga nchi yenye nguvu, yenye mafanikio na ya kidemokrasia.

"Ninaahidi kuwa mtiifu kwa Katiba ya Jamhuri ya Watu wa China (PRC), kulinda mamlaka ya Katiba, kutimiza wajibu wangu wa kisheria, kuwa mwaminifu kwa nchi na wananchi, na mwaminifu katika wajibu wangu, kukubali usimamizi wa wananchi na kufanya kazi kwa ajili ya nchi nzuri ya kisasa ya ujamaa ambayo ina ustawi, nguvu, demokrasia, usawa, na inayopendeza,” amesema Xi.

Xi Jinping achaguliwa tena kukiongoza chama cha kikomunisti China

Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa China, kwa upesi ilituma salamu za dhati kumpongeza Xi kwa kuchaguliwa tena.

Salamu hizo za Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa Rais Xi zilisema "Urusi inathamini sana mchango wako binafsi katika kuimarisha mshikamano wetu na ushirikiano wa kimkakati baina ya nchi zetu”.

Kuchaguliwa tena kwa Rais Xi ni kilele cha kupanda kwake, kutokea alipokuwa mwanachama mdogo wa chama hicho cha kikomunisti hadi kuwa kiongozi wa nchi yenye nguvu duniani.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amempongeza Rais Xi kwa kuchaguliwa tena kuwa rais wa China kwa miaka mingine mitano.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amempongeza Rais Xi kwa kuchaguliwa tena kuwa rais wa China kwa miaka mingine mitano.Picha: Alexandr Demyanchuk/Sputnik/AFP

Aidha kunamfanya kuwa rais mkomunisti wa China aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi, na inamaanisha anaweza kuendelea kutawala katika miaka yake ya sabini ikiwa hakutaibuka mpinzani yeyote dhidi yake.

Xi Jinping achaguliwa rais mpya wa China

Malengo ya kijasiri ya Xi kwa taifa lake, yamebadilika kuwa mtindo wa uongozi wake, huku maamuzi yakitekelezwa na maafisa ambao ni watiifu kwake ambao wanashikilia nyadhifa za juu serikalini katika kipindi cha muongo mmoja madarakani.

Na kwa kuwa alichukua madaraka wakati chama cha CCP kilionekana kuyumba, amefanya bidii kubadili mienendo ambayo ingetishia kudhoofisha umuhimu wa chama chake katika jamii ya China.

Kevin Rudd, waziri mkuu wa zamani wa Australia ambaye pia ni mtaalamu kuhusu masuala ya China, hivi karibuni alisema kuwa "Ajenda isiyokoma ya Rais Xi ya kudhibiti chama katika kila jambo, ingali hai".

(Vyanzo: AFPE, RTRE)