1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Xi Jinping achaguliwa rais mpya wa China

14 Machi 2013

Bunge la uteuzi nchini China limemteua kiongozi wa Chama cha Kikomunisti, Xi Jinping, kuwa rais hatua inayomuweka kwenye kilele cha madaraka ya taifa hilo linalokuwa kwa kasi kubwa ya kiuchumi duniani.

https://p.dw.com/p/17x9t
Newly-elected Chinese President Xi Jinping hold hands with former president Hu Jintao after the election of the new president of China during the12th National People's Congress (NPC) in the Great Hall of the People in Beijing on March 14, 2013. Chinese Communist Party leader Xi Jinping was named president of the world's most populous country after a vote at its parliamentary meeting in Beijing. AFP PHOTO /GOH CHAI HIN (Photo credit should read GOH CHAI HIN/AFP/Getty Images)
Xi Jinping Präsident Wahl China PekingPicha: GOH CHAI HIN/AFP/Getty Images

Xi Jinping aliinama kwa heshima juu ya jukwaa kuu katika Ukumbi Mkuu wa Watu wa China, kama linavyoitwa jengo la bunge la nchi hiyo, huku wajumbe wakimpigia makofi ya kumpongeza katika tukio hilo lililorushwa moja kwa moja na televisheni ya taifa.

Kati ya kura 2,961 zilizohisabiwa, ni kura moja tu iliyomkataa, huku wajumbe watatu wakiripotiwa kutokuhudhuria mkutano huo maalum wa uteuzi. Kwa hivyo, akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, Xi amepitishwa kwa asilimia 99.7 ya kura.

Tayari Xi alishachukua nafasi ya ukuu wa chama cha Kikomunsti kutoka kwa Hu hapo mwezi Novemba, na kabla ya kura ya leo kupigwa, mikutano ya awali ya viongozi wa kisiasa wa baraza hilo ilishalipitisha na kulipendekeza jina lake.

Kiongozi mkuu wa mambo yote

Sasa mwanasiasa huyo mwenye miaka 59 anatazamiwa kuwa rais na kiongozi mkuu wa chama kwa miaka 10 ijayo, ikiwa kila jambo litakwenda salama.

Xi Jinping akitembelea jeshi la China kaskazini magharibi mwa nchi hiyo mwezi Februari 2013.
Xi Jinping akitembelea jeshi la China kaskazini magharibi mwa nchi hiyo mwezi Februari 2013.Picha: picture alliance / landov

Katika mkutano huo, Li Yuanchao, ambaye ni mkuu wa Idara ya Oganaizesheni ya chama hicho cha Kikomunisti, ameteuliwa kuwa makamu wa rais, akiwa amepata asilimia 96 ya kura zilizohisabiwa.

Li, mwenye umri wa miaka 62 , ni mwalimu wa zamani wa skuli aliyejiunga na chama mwaka 1978, ambako alipanda ngazi haraka haraka kufikia nafasi ya kuongoza idara hiyo muhimu ya chama hapo mwaka 2007.

Pamoja na kuvikwa kofia mbili za uwenyekiti wa chama na urais wa nchi, wajumbe wa mkutano mkuu pia wamemuidhinisha Xi Jinping kuwa mwenyekiti wa kamisheni ya jeshi ya taifa, ikiwa ni nyongeza ya ukuu wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya Chama, ambao aliuchukua mwaka jana kutoka kwa Hu Jintao.

Hu aaga kwa mafanikio

Wote wawili, Hu na Xi, walipeana mikono ya pongezi mara mbili baada ya kutangawa kwa urais na nafasi ya kijeshi ya Xi, ingawa Xi hakuzungumza chochote juu ya uteuzi wake.

Rais mteule wa China Xi Jinping akiinama kwa heshima mbele ya mkutano mkuu wa bunge la nchi hiyo.
Rais mteule wa China Xi Jinping akiinama kwa heshima mbele ya mkutano mkuu wa bunge la nchi hiyo.Picha: Reuters

Hu, mwenye umri wa miaka 70, alijiuzulu nafasi zote za uongozi wa chama na urais, kutokana na sheria za China zinazohusu umri na kipindi ambacho kiongozi anaweza kuhudumu. Alikuwa ameshikilia nyadhifa hizo kwa miaka 10, akiwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo.

Hapo kesho, Ijumaa, mkutano huo mkuu wa Bunge la Watu wa China unatarajiwa kumthibitisha Naibu Waziri Mkuu Li Keqiang, ambaye kwa sasa anashikilia nafasi ya pili kwenye chama cha Kikomunsti, kuwa waziri mkuu akichukua nafasi ya Wen Jiabao.

Nafasi muhimu ya uwaziri wa mambo ya nje na zile za mawaziri wengine zitatangazwa hapo Jumamosi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman