1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaZimbabwe

Raisi azikosoa nchi za Magharibi kwa kuiwekea Iran vikwazo

14 Julai 2023

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amekamilisha ziara yake ya mataifa matatu barani Afrika na kutia saini mikataba kadhaa ya ushirikiano na serikali za Kenya, Uganda na Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/4Ts8B
Irans Präsident Ebrahim Raisi besucht Simbabwe
Rais wa Iran Ebrahim Raisi akikagua gwaride la heshima alipowasili kwenye uwanja wa ndege mjini Harare.Picha: JEKESAI NJIKIZANA/AFP

Rais wa Iran Ebrahim Raisi alikaribishwa kwa shangwe na watu kuimba nyimbo za kuzikosoa nchi za Magharibi alipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Robert Mugabe mjini Harare na kulakiwa na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.

Nchi zote mbili, Zimbabwe na Iran ziko chini ya vikwazo vya Marekani.

Soma pia: Raisi ayalaumu mataifa ya Magharibi kuchochea ushoga 

Wizara ya habari na mawasiliano ya Zimbabwe ilieleza kuwa Rais Mnangagwa na mwenzake wa Iran wanapania kushirikiana zaidi katika sekta za nishati, kilimo na mawasiliano.

Iran na Zimbabwe zimetia saini mikataba 12 yenye lengo la kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema, "Sisi wawili ni wahanga wa vikwazo vya nchi za Magharibi na tunazungumza baina yetu. Waliotuwekea vikwazo hivi hawataki tuzungumze, lakini kwa sababu sote ni wahanga ni muhimu kuwaonyesha kwamba tumeungana."

Iran yaieleza ziara hiyo kama "hatua muhimu" ya kuimarisha uhusiano

Kabla ya kuizuru Zimbabwe, Raisi alikuwa ameitembelea Kenya na Uganda ambapo pia alitia saini mikataba kadhaa ya ushirikiano na serikali ya Rais William Ruto na Rais Yoweri Museveni.

Irans Präsident Raisi beginnt eine Afrikareise durch drei Länder in Uganda
Rais wa Iran Ebrahim Raisi akisalimiana na Rais mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni katika Ikulu ya mjini Entebbe.Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Nchi zote tatu za Afrika zina uhusiano mzuri na Iran na wanaiona Jamhuri hiyo ya Kiislamu kama mshirika muhimu wa biashara, uwekezaji na pia zinashirikiana katika nyanja za sayansi, michezo na teknolojia.

Ilikuwa ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo wa Iran barani Afrika katika kipindi chake cha uongozi.

Ziara ya mwisho ya kiongozi wa Iran nchini Zimbabwe ilifanywa mnamo mwaka 2010 na Rais wakati huo Mahmoud Ahmadinejad.

Soma pia: Watu wawili wanyongwa kwa kushambulia eneo takatifu Iran

Iran inapania kunyoosha mkono wa urafiki kwa mataifa kadhaa duniani hasa wakati huu ambapo inakabiliwa na vikwazo vikubwa vya kimataifa kutokana na mpango wake wa nyuklia. Vikwazo vikali vya mataifa ya Magharibi dhidi ya Iran vinalenga hasa kuizuia nchi hiyo kutengeneza silaha za nyuklia.

Akiwa Harare, Raisi ameeleza, "Iran na Zimbabwe inapinga vikwazo dhidi yetu, tunaamini vikwazo hivyo vinatumiwa na Marekani kama silaha ya kijeshi dhidi ya mahasimu wao."

Tehran hata hivyo inasisitiza kuwa mpango wake wa nishati ya nyuklia unadhamiria kuzalisha umeme kwa wingi kwa ajili ya matumizi ya ndani.

Iranischer Präsident Ebrahim Raisi in Kenia
Rais wa Iran akikagua gwaride la heshima kabla ya kukutana na Rais wa Kenya William Ruto katika Ikulu mjini Nairobi.Picha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Katika ziara yake barani Afrika, Raisi alisisitiza haja ya mataifa hayo kutosafirisha mali ghafi kwa mataifa ya Magharibi. Akiwa Uganda, kiongozi huyo wa Iran alielezea uungwaji wake mkono kwa sheria kali inayopinga mapenzi ya jinsia moja.

Ameongeza kuwa, mataifa ya Magharibi yanaendekeza mapenzi ya jinsia moja na kushambulia misingi ya jadi ya familia chini ya kivuli cha kutetea haki za binadamu.

Yapata miezi miwili iliyopita, bunge la Uganda lilipitisha sheria kali ya kuharamisha ushoga na mapenzi ya jinsia moja.