Robert Zoellick ndiye rais mpya wa Benki ya dunia
30 Mei 2007Zoellick anachukua wadhifa huo baada kulazimika kujiuzulu kwa Paul Wolfowitz kufuatia sakata ya rushwa iliyokuwa inamkabili kwa muda wa wiki kadhaa.
Kutangazwa kwa Zoellick ambaye ni mtu shupavu katika masuala nyeti kuanzia biashara ya kimataifa hadi masuala yanayohusu mizozo kama vile Darfur, kuwa rais mpya wa Benki ya dunia kunaweza kuonekana kama rais Bush anatafuta hatimaye njia ya kuyazima manung’uniko yaliyokuwa yametawala kwenye benki ya dunia katika muda wa wiki kadhaa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangazwa kuongoza taasisi hiyo Robert Zoellick alisema chombo hicho kitajizatiti kupambana na hali ya umaskini.
Zoellick ameteuliwa baada ya kutolewa matokeo ya uchunguzi uliofanywa na jopo maalum la benki ya dunia ambao ulidhihirisha rais wa benki hiyo Paul Wolfowitz alikiuka maadili ya benki hiyo kwa kumpendelea mpenzi wake wa kike Shaha Riza kwa kumpandisha cheo na kuongezwa mshahara mnono.
Hatua hii ilizusha makelele sihaba huku miito ikitolewa kutoka kila upande kumtaka Wolfowitz ajiuzulu.
Wolfowitz amekubali kujiuzulu mnamo mwezi juni 30 kumaliza kelele hizo zilizokuwa zinatolewa kuanzia ndani ya taasisi hiyo ya kupambana na Umaskini hadi nje . Uteuzi wa Zoellick lakini utabidi kuidhinishwa na bodi ya magavana ya benki ya dunia yenye wanachama 24
Pamoja na yote lakini uteuzi wa bwana Zoellick huenda ukazusha maswali miongoni mwa nchi za ulaya ambazo zilivunjwa moyo na uteuzi uliofanywa na rais Bush mwaka 2005 wa bwana Wolfowitz, aliyewahi kuwa naibu wa waziri wa ulinzi na vile vile msanifu wa vita vya Iraq.
Bwana Zoellick pia mwenye umri wa miaka 53 aliunga mkono matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya aliyekuwa rais wa Iraq Saddam Hussein.
Zoellick aliwahi kuwa naibu wa waziri wa mambo ya nje Condolezza Rice mwezi Februari mwaka 2005 baada ya kuwa mwakilishi wa Marekani katika masuala ya biashara kwa miaka minne.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika utawala war ais Bush anasema uteuzi wa Zoellick unaweza kupokelewa vyema na nchi ambazo zilishauriwa na waziri wa fedha wa Marekani Henry Paulson aliyeongoza harakati za kumtafuta mrithi wa bwana Wolfowitz.
Afisa huyo lakini amekataa kuzitaja nchi hizo.
Afisa huyo ameongeza kusema Robert Zoellick mwenye tajriba ya muda mrefu katika masuala yanayohusu biashara ya kimataifa, fedha, na diplomasia ni mtu pekee aliyeweza kuonekana bora kuchukua wadhifa huu.
Na vile vile anaungwa mkono na kuheshimiwa na maafisa wengi duniani na pia anaamini kwa dhati lengo la benki ya Dunia la kupambana na umaskini.
Tayari mataifa ya ulaya yametoa maoni yao kuhusu uteuzi huo,waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner amesema Robert Zoellick lazima arudishe imani ya watu katika taasisi hiyo ya kupambana na umasikini.
Tangu jadi Marekani inamteua rais wa benki ya dunia lakini baadhi ya nchi wanachama wa benki hiyo na wabunge kadhaa wa Marekani wametoa mwito kwa utawala huo wa Marekani kukiweka wazi kinya’ng’anyiro hicho na kuvutia wagombea mbali mbali duniani baada ya sakata hii ya rushwa iliyomuandama Wolfowitz.