1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto kutoa maelezo The Hague.

Halima Nyanza5 Novemba 2010

Waziri wa Elimu ya Juu wa Kenya aliyesimamishwa kazi, William Ruto, leo anatoa taarifa rasmi katika mahakama ya kimataifa ya The Hague, kuhusiana na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu nchini humo mwaka 2007.

https://p.dw.com/p/PzPm
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Uhalifu ya Kivita ICC ya mjini The Hague, Luis Moreno Ocampo.Picha: AP

Bwana William Ruto ameyasema hayo jana wakati alipokutana na Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, Luis Moreno-Ocampo na kwamba hii leo watakutana tena kwa mazungumzo.

Bwana Ruto ambaye aliwasili nchini humo humo jana akitokea Kenya, alinukuliwa na vyombo vya habari vya nchini mwake akisema kwamba anataka kutoa ushahidi wake kwa mahakama hiyo, ambayo inachunguza machafuko yaliyosababisha umwagaji damu nchini Kenya ambapo kiasi cha watu 1,300 waliuawa.

Hata hivyo ofisi ya Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo ya ICC, haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na kauli hiyo ya Ruto.

Mahakama hiyo ya ICC, mpaka sasa bado haijawataja washukiwa muhimu, lakini Tume ya Haki za Binadamu nchini Kenya imesema Waziri huyo alihusika katika kutokea kwa mapigano hayo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 nchini humo.

Aidha Majaji nchini Kenya pia walizuia jaribio la Makamu Waziri mkuu na Waziri wa fedha wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta, kuondoa jina lake katika ripoti iliyotolewa.

Awali mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Luis Moreno-Ocampo aliarifu juu ya lengo la kutoa waranti wa kukamatwa kwa viongozi waliohusika kupanga mauaji hayo nchini Kenya na kwamba kukamilisha kusikilizwa kwa mashahidi kutamalizika mwishoni mwa mwaka ujao wa 2011, huku kesi ikitarajiwa kuanza kusikilizwa mwishoni mwa mwaka 2012, mwaka ambao nchi hiyo itafanya uchaguzi mkuu.

Hatua hiyo ya William Ruto kuamua kwenda mwenyewe The Hague, imepongezwa na maafisa wa serikali ya Kenya na kusema kuwa ni mfano kwa wengine, ambao pengine nao wanachunguzwa.

Lakini Msemaji wa Waziri Mkuu wa Kenya, Dennis Onyango amesema, Waziri Mkuu Raila Odinga amechukulia uamuzi huo wa Ruto kama ni uamuzi binafsi na kwamba yeye hana shida na hilo.

Nao wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wanasema kuwa waranti wowote utakaotolewa dhidi ya mawaziri wa Kenya unaweza kuleta mpasuko mkubwa katika serikali ya mseto inayoongozwa na Rais Mwai Kibaki na kusababisha machafuko katika maeneo wanakotoka watuhumiwa hao.

Kwa upande wake Profesa Macharia Munene, mhadhiri wa uhusiano wa kimataifa katika chuo kikuu cha Kimarekani nchini Kenya, USIU, alikuwa na mtazamo huu, juu ya hatua ya William Ruto kujipeleka mwenyewe The Hague.

William Ruto pia anakabiliwa na mashtaka mengine, nchini mwake. Alisimamishwa kazi mwezi uliopita kwa tuhuma za rushwa, ambazo binafsi amezikanusha na atapanda kizimbani nchini Kenya dhidi ya mashtaka hayo kuanzia mwishoni mwa mwezi Januari, mwakani.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)

Mhariri:Josephat Charo