Rwanda yaiomba Malawi kuwakamata washukiwa wa mauaji
6 Juni 2023Serikali ya Malawi imesema kuwa Rwanda imeiomba kusaidia kuwakamata washukiwa 55 wanaosakwa kuhusiana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambao wanaaminika kujificha nchini humo. Waziri wa Usalama wa Malawi Ken Zikhale Ng'oma amesema serikali ya Kigali imewasilisha ombi rasmi la usaidizi wakati ikitafuta mahali walikojificha washukiwa hao wanaofahamika pia kama "wababe wa kivita".
Washukiwa wanaodaiwa kujificha nchini Malawi wanasakwa kuhusiana na "vifo vya zaidi ya watu 2,000 katika baadhi ya makanisa. Ombi la Rwanda linajiri wiki kadhaa baada ya kukamatwa nchini Afrika Kusini mshukiwa Fulgence Kayishema ambaye amekuwa akisakwa kwa zaidi ya miongo miwili na ambaye mara kadhaa amekuwa akitumia pasipoti ya Malawi. Wakati wa mauaji hayo ya kimbari yaliyodumu siku 100, takriban Wanyarwanda 800,000, wengi wao wakiwa Watutsi waliuawa na Wahutu wenye msimamo mkali.