Rwanda yakanusha madai ya Kongo dhidi ya kampuni ya Apple
27 Aprili 2024Matamshi ya Rwanda yametolewa baada ya Kongo kuishtumu kampuni hiyo kwa kutumia kwenye bidhaa zake, madini yanayosafirishwa kinyume cha sheria kutoka nchini humo.
Hapo jana Ijumaa, msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba hii ni hatua ya hivi karibuni zaidi ya serikali ya Kongo ambayo inajaribu kwa mara nyingine kuiangazia Rwanda kwa shtuma za uongo.
Soma pia: Umoja wa Mataifa waonya kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama Mashariki mwa Kongo
Siku ya Alhamisi, mawakili wa Kongo waliishtumu kampuni ya Apple kwa kununua madini yaliochimbwa kutoka mashariki mwa nchi hiyo na kuingizwa nchini Rwanda kinyume cha sheria, ambapo baadaye husafishwa na kuingizwa katika soko la kimataifa.
Mawakili hao waliwasilisha notisi rasmi kwa Apple ya kuionya kwamba huenda ikakabiliwa na hatua za kisheria ikiwa itaendelea kununua madini hayo.