UN: Hali ya usalama yaendelea kuzorota mashariki mwa DRC
28 Machi 2024Bintou Keita ameyasema hayo kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hiyo jana na kusisitiza kuwa kundi la waasi lenye mafungamano na nchi jirani ya Rwanda, limekuwa likipiga hatua zaidi ili kutanua eneo lake la udhibiti, jambo ambalo amesema limesababisha hali mbaya ya kibinaadamu na kupelekea kuongezeka kwa idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.
Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood amelaani "uvamizi wa kijeshi" mashariki mwa Kongo unaoendeshwa na waasi wa M23 pamoja na Jeshi la Ulinzi la Rwanda huku akikemea mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Balozi Wood amewatolea wito viongozi wa Rwanda na Kongo kuchukua hatua za kuendeleza mchakato wa amani kwa manufaa ya watu wao, ukanda mzima na dunia kwa ujumla.