1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari za ndege kufutwa katika viwanja vya Brussels

Josephat Charo
1 Oktoba 2024

Safari zote za kibiashara kutoka viwanja viwili vikubwa vya ndege nchini Ubelgiji zitafutwa hivi leo kwa sababu ya mgomo wa maafisa wa usalama. Hayo yamesemwa na kampuni mbili zinazosimamia shughuli katika viwanja hivyo.

https://p.dw.com/p/4lGVw
Safari za ndege katika viwanja viwili vya mjini Brussels zitafutwa
Safari za ndege katika viwanja viwili vya mjini Brussels zitafutwaPicha: Cristof Stache/AFP

Mgomo huo unaoviathiri viwanja vya Brussels-Zaventem na Charleroi, umeitishwa na muungano wa vyama vya wafanyakazi kulalamika kuhusu hali mbaya ya mazingira ya kazi katika sekta ya usafi, usalama na upishi.

Maandamano yamepangwa kufanyika leo mchana mjini Brussels katika eneo lenye afisi za Umoja wa Ulaya ili kuutanabahisha umoja huo kuhusu masuala hayo. Katika uwanja wa Brussels-Zaventen, ambao ndio mkubwa kabisa nchini Ubelgiji, safari zote 249 zilizopangwa kuondoka, zimefutwa, huku ndege 98 tu kati ya 243 zilizopangwa kutua, zitaweza kutua.

Katika uwanja wa Charleroi, takriban safari 100 za ndege ziilizopangwa kuondoka, zimefutwa lakini ndege zilizopangwa kutua hazijaathiriwa.

Kuondoka kwa ndege kunazuiwa na kutokuwepo wapekuzi wa mizigo ambao huduma zao katika viwanja vyote viwili hufanywa na kampuni kubwa ya kimataifa ya Uingereza G4S.

Maalfu ya abiria walioathiriwa na kufutwa kwa safari za ndege watapata mawasiliano kutoka kwa mashirika ya ndege wanayosafiria.