Scholz asema shambulizi la kisu Solingen ni ´ugaidi´
26 Agosti 2024Scholz amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Solingen kwamba shambulizi hilo lilikuwa ni la kigaidi na lililotishia jinsi watu wanavyoishi kwa umoja.
Scholz aliyeambatana na maafisa waandamizi wa kisiasa alisisitiza kuanzisha hatua za kuimarisha sheria za silaha na hasa matumizi ya visu, na kuahidi kufanya liwezekanalo kuhakikisha wale wasioweza kuishi Ujerumani, wanarejeshwa.
"Tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba wale wote ambao hawawezi kuishi hapa Ujerumani wanarejeshwa makwao kwa kutumia kanuni za kisheria ambazo tumekubaliana hivi karibuni."
Shambulizi hilo limezusha mjadala kuhusu uhamiaji nchini Ujerumani. Mtuhumiwa wa shambulizi hilo, raia wa Syria alijisalimisha Jumamosi jioni na kukiri, baada ya kujificha kwa siku nzima.