Seneta wa Meru kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za uchochezi
10 Januari 2022Seneta Mithika Linturi alikamatwa mjini Eldoret mapema jana na kusafirishwa hadi Nakuru na muda mfupi baadaye kusafirishwa hadi jijini Nairobi kufuatia agizo la maafisa wa ujasusi. Inaaminika alirejeshwa usiku mjini Nakuru na kulala korokoroni akisubiri kufunguliwa mashtaka hii leo.
Kwenye mkutano wa Eldoret Linturi alisikika akihoji namna watu wa eneo la mlima Kenya wamesimama na naibu Rais ilhali kunao wanaoishi maeneo ya bonde la ufa ambayo ni ngome yake, wasiomuunga mkono, na hivyo akawataka waondoe madoadoa kati yao. Kupitia wakili wake Elias Mutuma, Linturi amesema leo hii kuwa matumizi ya neno madoadoa sio uhalifu chini ya sheria ya Kenya.
"Kwenye sheria zetu nchini neno madoadoa halijapigwa marufu au kuelezewa kutokuwa halali kwa hivyo sio sawa kwa mtu yeyote kutoa shtaka kama hilo. Linturi alikuwa anawahimiza watu wa Eldoret kupiga kura kwa pamoja.” alisema Mutuma.
Soma pia:Kamishna wa magereza Kenya ashitakiwa
Makovu ya machafuko ya mwaka 2017
Matamshi ya kiongozi huyu yameibua hisia kali, viongozi wa kitaifa na wanasiasa wakilaani kauli kama hizi wanazoamini zinatishia mshikamano wa taifa. Neno madoadoa linaleta kumbukumbu mbaya na linachukuliwa na uzito mwingi kati ya jamii za eneo la bonde la ufa, kwani lilitumika kuhimiza ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 zilizosababisha maafa makubwa eneo hili.
Waziri wa ulinzi wa Kenya Eugene Wamalwa ameitaka tume ya uchaguzi nchini IEBC kuzingatia swala la maadili kati ya wanasiasa wanaogombea viti.
Soma pia :Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta asema Afrika iko njia panda
Njama ya kisiasa ?
Wanasiasa walio kwenye mrengo wa naibu Rais wanalalamika kwamba wanalengwa kisiasa. Seneta wa Nakuru Susan Kihika akiwashutumu polisi kwa kutumia misingi tofauti ya kisheria dhidi yao.
Maafisa kutoka tume ya uwiano na utangamano nchini pamoja na maafisa wa ujasusi wanaongoza uchunguzi huu. Mkurugenzi wa mashataka ya umma nchini ameagiza Inspekta mkuu wa polisi kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha ripoti kwake kufikia tarehe 14 mwezi huu.