Ujerumani yaweka kanuni mpya za kuzuia maambukizi ya corona
22 Desemba 2021Nchini Ujerumani viongozi wa shirikisho na serikali ya mnamo siku ya Jumanne walipitisha kwa kauli moja kwamba kuanzia wiki ijayo sheria ya kuzuia mikusanyiko itaanza kwa watu wote ikiwa ni pamoja na wale waliochanjwa au waliopona ugonjwa wa COVID -19.
Kanuni hizo zitakazoanza kutumika Desemba 28 zinalenga kuwazuia watu kuhudhuria sherehe kubwa za mkesha wa Mwaka Mpya huku kukiwa na wasiwasi juu ya kuongezka kwa virusi vipya vya omicron. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema sasa sio wakati wa watu kusherehekea wakiwa kwenye makundi makubwa.
Wataalamu wa matibabu nchini Afrika Kusini wamesema maambukizi ya corona yameshuka kwa kiasi kikubwa hali ambayo inaashiria kwamba nchi hiyo imevuka kilele cha maambukizi ya virusi vipya aina ya omicron. Hata hivyo watalaamu hao wa afya wamesema hali hiyo inaweza pia kuwa ni kwa sababu ya kutokuwepo data za kuaminika kuhusu idadi ya kila siku ya watu walioambukizwa, hali inayosababishwa na upimaji usio sawa au kuchelewesha kuripoti mabadiliko mengineyo lakini wamesema maambukizo ya omicron yanaweza kuwa yamepungua haraka baada ya kuongezeka kwa kasi katika siku za hivi karibuni.
Israel kwa upande wake imetangaza kwamba itatoa chanjo ya nne dhidi COVID-19 kwa watu walio na umri wa zaidi ya miaka 60, huku kukiwa na wasiwasi nchini humo juu ya kuenea kwa aina mpya ya virusi vya corona, Omicron. Jopo la wataalamu wa Wizara ya Afya nchini humo wamependekeza chanjo hiyo ya nne, uamuzi ambao umepokelewa kwa haraka na Waziri Mkuu Naftali Bennett. Bennett amewataka Waisraeli kupata chanjo hiyo haraka iwezekanavyo.
Nchini Marekani meya wa Jiji la New York Bill de Blasio ametangaza motisha ya dola 100 kwa wakazi watakaopata chanjo ya nyongeza dhidi ya COVID-19. Virusi vya aina ya Omicron, ambavyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza mwezi uliopita sasa vimewaathiri asilimia 73 ya Wamarekani na vimesababisha maambukizo kuongezeka maradufu katika muda wa siku 1 hadi siku 3, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni WHO.
Chanzo:/DW